Morogoro. Jeshi la Polisi mkoani Morogoro, linamsaka Helakumi Kacheri kwa tuhuma za kumuua mkewe, Sofina Elipisini (27), mkazi wa Singisa, wakiwa shambani, huku chanzo kikidaiwa kuwa wivu wa kimapenzi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama, amesema mtuhumiwa alimuua mkewe kwa kumshambulia na silaha yenye makali sehemu mbalimbali za mwili, akimtuhumu kuendeleza uhusiano na mzazi mwenzake wa awali.
Amesema baada ya mtuhumiwa kutekeleza mauaji hayo, alikimbia, na Jeshi la Polisi linaendelea kumsaka ili afikishwe kwenye vyombo vya sheria.
Diwani wa Singisa, Anna Mgela, amesema tukio hilo limetokea Januari 4, 2026 katika kitongoji cha Tindegela, kata ya Singisa, wilayani Morogoro, na kwamba alipata taarifa kutoka kwa mtendaji wa kijiji walichokuwa wakiishi.
“Nikiwa kwenye kikao, nilipigiwa simu na mtendaji wa kijiji na kunipa taarifa za mauaji haya, sikuweza kufika eneo la tukio, badala yake nilimuagiza mtendaji atoe taarifa polisi. Baada ya polisi kufika, waliuchukua mwili. Hata hivyo, mtuhumiwa hakupatikana kwa sababu baada ya kufanya hivyo alikimbia,” amesema Mgela.
“Hawa wanandoa nawafahamu. Huyu mwanamke, ambaye kwa sasa ni marehemu, awali alikuwa na mume wa ndoa na alizaa naye watoto wawili wa kike, lakini waliachana.
“Akaolewa tena na huyu mtuhumiwa, na mwanaume akaoa mwanamke mwingine, lakini sifahamu kama baadaye walirudiana kimapenzi, wala sijui kama mwanaume wa sasa alikuwa na ugomvi na mkewe (marehemu),” amesema Mgela.
Ameongeza: “Tukio hili la mauaji limetuumiza wananchi wa Singisa, na mimi binafsi usiku wa jana sijalala vizuri. Kila nikishtuka, nawaza hili tukio kwa sababu nawafahamu, nawaza kimetoa nini mpaka mwanaume kaamua kuchukua uamuzi huu wa kumuua mke wake kinyama hivi.”
Mgela amesema baada ya tukio hilo, amepanga kuzungumza na wenyeviti wa vijiji na kuweka ajenda maalumu ya ulinzi na usalama, ambayo itajadiliwa kwenye vikao vya Baraza la Maendeleo ya Kata (BMK). Kupitia vikao hivyo, wananchi watatakiwa kueleza changamoto zitakazowakabili, zikiwemo zile za mahusiano ya ndoa na kifamilia.
Mbali na tukio hilo, Kamanda Mkama amesema polisi wanafanya uchunguzi wa kifo cha Jese Melumba (49), anayedhaniwa kujiua kwa kunywa sumu ya kuulia magugu shambani.
Tukio hilo limetokea Januari 4, 2026 asubuhi katika kitongoji cha Isago, kata ya Mngeta, Wilaya ya Kilombero, na uchunguzi wa awali umebaini kuwepo kwa mabaki ya dawa hiyo nyumbani kwake.
Katika tukio jingine, Kamanda Mkama amesema, ni la kifo cha Ally Dagaza (38), mkazi wa kitongoji cha Doma Stendi, kata ya Doma, wilayani Mvomero, aliyefariki dunia akiwa shambani kwake baada ya kukanyagwa na tembo.
