KIUNGO wa Shamakhi FC, Alphonce Mabula amesema kucheza michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) akiwa na kikosi cha Taifa Stars kumeanza kumpa uzoefu wa mechi za kimataifa na somo kwenye soka.
Mabula aliyeitwa kwa mara ya kwanza kwenye kikosi cha Taifa Stars, alicheza mechi zote tatu za hatua ya makundi kwa dakika 90 akianza dhidi ya Nigeria ambapo Tanzania ilipoteza kwa mabao 2-1, kisha sare ya 1-1 dhidi ya Uganda na Tunisia.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mabula amesema kushiriki AFCON na kuiwezesha Tanzania kufuzu hatua ya 16 bora ni rekodi kubwa na historia muhimu katika maisha yake ya soka.
Aliongeza pamoja na rekodi hiyo lakini amejifunza vitu vingi kupitia wachezaji mbalimbali waliomzidi uzoefu.
“Ni fahari kubwa kwangu kucheza AFCON kwa mara ya kwanza na kuandika historia ya kuisaidia Tanzania kufika hatua ya 16 bora. Hili ni jambo ambalo sitolisahau ukizingatia nikiwa na umri mdogo naandika rekodi hiyo,” amesema Mabula.
Aliongeza kuwa pamoja na mafanikio hayo, amejifunza mambo mengi ikiwemo nidhamu na nguvu ya upambanaji kupitia wachezaji wanaocheza ligi kubwa duniani akimtolea mfano nahodha Mbwana Samatta anayekipiga Le Havre ya Ufaransa.
“Hii michuano imenipa somo kubwa kucheza dhidi ya wachezaji wakubwa wa Afrika kunakujenga kisaikolojia na kiufundi.”
