USHINDI wa mabao 2-1 ilioupata Azam dhidi ya URA wafungaji wakiwa Jephte Kitambala na Albogast Kyobya, yameifanya timu hiyo kumaliza kinara wa kundi A.
Kwa kumaliza kinara ikiwa na pointi saba, Azam sasa imefuzu nusu fainali ikisubiri kukutana na Simba au Fufuni itakayoongoza kundi B.
Katika mechi ya leo Januari 5, 2026 iliyochezwa Uwanja wa New Amaan Complex, URA ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia Nelson Ssenkatuuka dakika ya 10 akiunganisha pasi ya Aliro Moses.
Kuingia bao hilo, kukaongeza presha kwa Azam ambayo ilijipanga kikamilifu kuona inafanyaje isawazishe.
Wakati Azam ikipambana kusawazisha, dakika ya 23 beki wa kulia wa timu hiyo, Nathaniel Chilambo akarusha mpira uliomkuta Jephte Kitambala akiwa ndani ya boksi, akageuka na kuachia shuti kali, mpira ukatikisa nyavu za juu za URA. Matokeo yakawa 1-1 hadi kipindi cha kwanza kinamalizika.
Kipindi cha pili, mabenchi ya ufundi ya timu zote mbili yalikuwa yakikuna vichwa kuona namna gani ushindi unapatikana ambapo URA ilihitaji zaidi ushindi ili kufuzu nusu fainali, wakati Azam sare tu ingewabeba.
Mabadiliko ya wachezaji kipindi cha pili, yaliinufaisha zaidi Azam kwani Albogast Kyobya aliyeingia dakika ya 84 kuchukua nafasi ya James Akaminko akafunga bao la ushindi dakika ya 90+4.
Bao hilo lilitokana na Azam kufanya shambulizi la kushtukiza baada ya URA kulivamia lango la Azam na kuweka kambi kwa muda ikisaka ushindi.
Mpira mrefu uliomkuta Ngita Kamanya wa Azam aliyeingia dakika ya 90 kuchukua nafasi ya Jephte Kitambala, aliutumia vizuri kumpasia Albogasti akiwa pembeni kidogo ya boksi la URA, akaachia shuti lililogonga mwamba wa pembeni kwa chini na kujaa wavuni.
Ushindi huo umeifanya Azam kumaliza kinara wa kundi A ikisubiri kucheza nusu fainali dhidi ya atakayekuwa kinara kundi B kati ya Simba yenye pointi tatu na Fufuni yenye pointi moja ambazo zinakutana baadae saa 2:15 usiku.
Hiyo itakuwa nusu fainali ya kwanza itakayochezwa Januari 8, 2026 saa 2:15 usiku kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, kisha Januari 9, 2026 uwanjani hapo itapigwa nusu fainali ya pili kati ya Singida Black Stars na kinara wa kundi C kati ya Yanga na TRA United zitakazokutana kesho Jumanne kumaliza ubishi.
