Beki Mkongomani anukia Dodoma Jiji

UONGOZI wa Dodoma Jiji umeanza maboresho ya kikosi hicho katika dirisha hili dogo lililofunguliwa rasmi Januari Mosi, ambapo kwa sasa unakaribia kuipata saini ya beki wa kati raia wa DR Congo, Herve Beya Beya, ili kwenda kuongezea nguvu.

Beki huyo aliyezaliwa Machi 31, 1999, kwa sasa anaichezea timu ya OC Bukavu Dawa ya DR Congo aliyojiunga nayo Agosti 17, 2024, akitokea CS Don Bosco, ambapo mabosi wa Dodoma Jiji wako katika hatua za mwisho za kuipata saini yake.

Chanzo kutoka ndani ya uongozi wa timu hiyo, kimeliambia Mwanaspoti, uongozi wa beki huyo ulikuwa Tanzania kwa ajili ya kukamilisha baadhi ya taratibu za kujiunga na kikosi hicho, ambapo mazungumzo hayo yameenda vizuri kati ya pande mbili.

BE 01

“Kila kitu kinaenda vizuri na mambo yaliyobakia ni madogo tu ambayo kwa siku hizi mbili zijazo tutayakamilisha, ni beki mzoefu aliyecheza Ligi mbalimbali, ambapo tunaamini ataongeza utulivu katika eneo la kujilinda,” kilisema chanzo hicho.

Beya amewahi pia kucheza timu mbalimbali zikiwamo za AS Nyuki na AS Maniema Union zote za DR Congo na Gasogi United ya Rwanda, ambapo beki huyo anatazamiwa kuongeza ushindani katika eneo la kulinda la kikosi hicho cha ‘Walima Zabibu’.

BE 02

Mbali na beki huyo, Mwanaspoti linatambua pia Dodoma Jiji inakaribia kukamilisha usajili wa mshambuliaji mwingine wa DR Congo, Osako Ngeleda Modeste, ambapo dili hilo linaenda vizuri na muda wowote atatambulishwa kukichezea kikosi hicho.

Modeste ni nyota aliyecheza timu mbalimbali za AS Vita Club ya DR Congo, Cape Town Spurs ya Afrika Kusini, Clube Recreativo Desportivo do Libolo, Grupo Desportivo Interclube, Atletico Sport Aviacao na Santa Rita de Cassia za Angola.