Chukwu, Yakoub hawashikiki Mapinduzi Cup

KABLA ya jana jioni Yanga haijacheza dhidi ya KVZ, kuna mastaa wawili katika michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026 walikuwa wamefunika kwa kubeba tuzo nyingi.

Mastaa hao ni Morice Chukwu wa Singida Black Stars na Yakoub Said Mohamed ambao katika mechi za hatua ya makundi, kila mmoja amebeba tuzo mbili.

Chukwu ambaye anacheza eneo la kiungo katika kikosi cha Singida kilichofuzu nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi 2026, ndiye mchezaji pekee aliyebeba tuzo mbili za mchezaji bora wa mechi.

Mnigeria huyo amefanya hivyo katika mechi mbili kati ya tatu alizocheza ambapo alianza kubeba tuzo dhidi ya Mlandege wakati Singida ikishinda 3-1, kisha dhidi ya URA katika sare ya 1-1.

Kwa upande wa Yakoub, amebeba tuzo ya mchezaji aliyeonyesha mchezo wa kiungwana ‘Fair Play’ ambapo aliibuka kidedea dhidi ya Fufuni katika sare ya 1-1 na walipopokea kichapo cha 1-0 dhidi ya Simba.

Katika kuonyesha mfanano wa mastaa hao, tuzo zao wamebeba mechi ya kwanza na ya mwisho hatua ya makundi huku Chukwu akiisaidia Singida kufuzu nusu fainali, wakati Yakoub chama lake likitolewa.

“Tuzo hii inanifanya nizidi kupambana kuonyesha ubora wangu, nataka niendelee kuwa bora si Mapinduzi Cup tu, hata Ligi Kuu ya Tanzania.

“Siri ya ubora wangu ni kushirikiana na wenzangu kwani bila wao kwangu si kitu, ushirikiano tulionao matunda yake ndio haya,” amesema Chukwu.

Naye Yakoub amesema: “Hii inanipa picha kwamba natakiwa kusimamia nidhamu niliyonayo, kupewa tuzo mbili za mchezo wa kiungwana katika mechi mbili tofauti sio kitu kidogo. Nashukuru sana kwa waandaaji wa tuzo hii.”