Dabi ya Mzizima yanukia nusu fainali Mapinduzi Cup

LEO Jumatatu, makundi mawili katika Kombe la Mapinduzi 2026 yanamaliza mechi zake ambapo baada ya dakika tisini, tunaweza kushuhudia jambo kubwa sana.

Nalo si jingine bali mechi ya nusu fainali inayoweza kuzikutanisha Azam dhidi ya Simba endapo tu timu hizo zote leo zitaibuka na ushindi.

Ipo hivi. Leo saa 10:15 jioni, Azam inacheza na URA katika mechi ya kundi A ambayo yeyote atakayeshinda anafuzu nusu fainali akiwa kinara wa kundi. Anaungana na Singida Black Stars iliyotangulia baada ya kufikisha pointi tano. Kumbuka Azam na URA zote zina pointi nne.

Baada ya mechi hiyo, saa 2:15 usiku, Simba itapambana na Fufuni, ni mechi ya kundi B. Zote hizi zitachezwa Uwanja wa New Amaan Complex.

Simba iliyoanza na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Muembe Makumbi, sare au ushindi inatosha kufuzu nusu fainali, lakini Fufuni ili ifuzu hatua hiyo, lazima ishinde kwani ina pointi moja hivi sasa iliyopata katika sare ya 1-1 dhidi ya Muembe Makumbi.

DAB 01

Kwa mujibu wa ratiba ya michuano hiyo, nusu fainali ya kwanza itakayochezwa Januari 8, 2026 majira ya saa 2:15 usiku kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja, itamkutanisha  Januari 8, 2026 timu kinara wa kundi A dhidi ya kinara Kundi B.

Hadi sasa, kinara kundi A ni Singida Black Stars, lakini Azam ikiichapa URA, basi itakaa juu wakati kundi B linaongozwa na Simba yenye nafasi kubwa ya kufuzu nusu fainali.

Hali ikiwa hivyo, basi tutashuhudia Mzizima Dabi ikipigwa katika Kombe la Mapinduzi, ambapo mara ya mwisho timu hizo zimekutana Desemba 7, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar katika Ligi Kuu Bara na Azam ikashinda 2-0.

Akizungumzia mechi yao dhidi ya URA, kocha mkuu wa Azam, Florent Ibenge amesema haitakuwa rahisi kwani amewaona wapinzani wake na anatarajia itakuwa mechi ngumu.

DAB 02

“Tunataka kucheza nusu fainali, kundi letu tunapita timu mbili, hivyo mechi ya mwisho ni lazima kushinda licha ya kwamba haitakuwa rahisi,” amesema Ibenge.

Kwa upande wa Ssemuyaba Bashir ambaye ni kocha msaidizi wa URA, amesema: “Itakuwa mechi ya kufa au kupona kati yetu na Azam, tunajiandaa na hiyo vita, tunataka kushinda na kuendelea hatua inayofuata.”

Kocha mkuu wa Simba, Steve Barker, kwanza amewapongeza vijana wake kwa ushindi wa mechi ya kwanza dhidi ya Muembe Makumbi, huku akibainisha kuwa imeongeza kitu kuelekea mechi ya leo dhidi ya Fufuni.

“Jambo zuri tumeshinda mechi ya kwanza, hivi sasa tunaangalia mbele ambapo tunahitaji pia kushinda,” amesema Barker.

DAB 03

Kocha wa Fufunu, Suleiman Mohamed ‘Mani Gamera’ , amesema: “Mtawala wa Tanzania Bara ni Simba, lakini mtawala wa Unguja ni Fufuni, tukikutana ndani ya uwanja itaamuliwa nani mtawala wa jumla.

“Haya ni mashindano makubwa, hatuwezi kuja kinyonge. Fufuni tuna malengo ya kufika fainali na kwenda kuchukua ubingwa ardhi ya nyumbani kule Pemba.”