Damaro, Tchakei, Mwanengo walivyoyaanza maisha mapya Yanga

PALE Yanga kuna majembe mapya matatu. Emmanuel Mwanengo kutoka TRA United, Marouf Tchakei na Mohamed Damaro waliotokea Singida Black Stars.

Majembe hayo yameanza kazi rasmi yakicheza mechi ya kwanza katika Kombe la Mapinduzi 2026, michuano inayoendelea kwenye Uwanja wa New Amaan, Unguja.

Katika mechi ya juzi dhidi ya KVZ ambayo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-0, majembe hayo yaliuwasha moto kila mmoja kwa nafasi yake.

Mwanengo ambaye alianzishwa eneo la ushambuliaji akiwa ndiye mshambuliaji kinara, alimaliza dakika zote tisini.

Damaro na Tchakei walitokea benchini, akianza kuingia Damaro dakika ya 61 akitolewa Duke Abuya, kisha dakika ya 76, Tchakei akachukua nafasi ya Celestin Ecua.

Mwanaspoti lilishuhudia mechi hiyo na hapa linakuchambulia kile walichofanya mastaa hao kwa muda walioupata.

WANA 01

Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves alimwanzisha Mwanengo kuwa mshambuliaji kinara katika mfumo wa 4-3-3, kisha baadaye alipobadilisha na kuwa 4-4-2, bado alibaki kuwa mshambuliaji wa mwisho.

Katika dakika tisini alizocheza Mwanengo, alihusika kwenye bao la mwisho ambapo mpira wake wa krosi iliyokuwa inakwenda kwa Pacome Zouzoua, ukakutana na beki wa KVZ, Rahim Andrea, akaubadilisha mwelekeo na kujaa wavuni akimpoteza maboya kipa wake, Bashir Muslim.

Mbali na bao hilo la dakika 75, Mwanengo alionekana kuwa mtulivu ndani ya boksi kwani katika mara tano alizopokea mpira akiwa eneo hilo, alipoona hana uwezo wa kulenga lango, anaachia pasi.

Kwa ujumla, dakika zake tisini pasi yake moja tu aliyopiga ndio ilipotea, huku nyingine 21 zikifika kwa walengwa ambazo asilimia kubwa zilikuwa fupi.

Shuti moja alilopiga lilitoka nje ya boksi, huku akifanikiwa kuwania mpira wa juu mara moja ambapo kichwa alichopiga, hakikulenga goli.

Faulo mbili alicheza kwa muda wote wa mechi, huku akifanikiwa kupokonya mpira mara moja.

Licha ya kuwa mshambuliaji wa mwisho, lakini kutokana na uwezo wake wa kucheza eneo la kiungo, Mwanengo alikuwa akishuka chini na kuifuata mipira kutoka kwa wenzake.

WANA 02

Dakika ya 61, Pedro anamuinua Damaro, kisha anamuita nje nahodha aliyekuwa akikiongoza kikosi cha Yanga dhidi ya KVZ, Duke Abuya ambaye majukumu yake ya unahodha anamuachia kipa Aboutwalib Mshery.

Kuingia kwa Damaro, kulizidi kuliweka eneo la kiungo katika utulivu mkubwa baada ya hapo awali Duke kupambana na viungo wa KVZ, Majid Khamis na Mussa Majuto.

Katika dakika 29 alizotumia nyota huyo, alifeli katika kitu kimoja pekee, kupiga pasi za mbali kwani mbili zote zilipotea kwa kutoka nje ya uwanja.

Hata hivyo, alionekana kuwa mzuri wa kupiga pasi za karibu kwani hakupoteza hata moja kati ya 33 alizogongeana na wenzake.

Mara moja alipokonya mpira kwa usahihi, huku akicheza faulo moja dakika ya 85 kwa Hassan Kassim.

YANG 03

Pasi zake alizokuwa anapiga ni kama za kuwachonganisha mabeki au kuwatamanisha watoke maeneo yao kwani zilikuwa zikipita katikati ya wachezaji wawili kumfikia nyota mwenzake wa Yanga.

Pasi hizo alikuwa anazipiga kwa juu staili ya mkunjo, lakini zingine akizitambaza chini.

Katika pasi hizo, Tchakei alikosea mara mbili, huku 11 zikitiki. Hakuwa mtu wa kupambania mipira ya juu, lakini ile ya chini aliipata mitatu. Hakupiga shuti lolote lililolenga lango la wapinzani.

WANA 03

Kocha mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves ameonekana kufurahishwa na viwango vya wachezaji hao, lakini akasema kuna kitu cha kuongeza hasa kwa Mwanengo.

“Nina furaha kwa sababu kuna wachezaji wamecheza kwa mara ya kwanza na kufanya vizuri wakiwamo wawili kutoka timu ya vijana. Ninju (Abubakar Othuman) na George (Mzungu). Pia Damaro, Tchakei na Mwanengo. Wote wamefanya vizuri. Nimependa.

“Mwanengo ana wasifu wa kucheza kama winga, ni vizuri zaidi kwa sababu ni kawaida kwake kujifunza. Lakini pia anaweza kucheza kama mshambuliaji katika mfumo wa 4-4-2 au 4-3-3. Ana ujuzi mzuri.

“Kwa mechi hii nilimpa malengo yake, lakini tunakwenda hatua kwa hatua. Yote kwa yote nimeridhishwa na kiwango chake,” amesema Pedro aliyerithi kiti cha Romain Folz.