Maswa. Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk Vincent Anney, amewaonya watu wanaovamia maeneo ya vyanzo vya maji na kufanya shughuli za kibinadamu, ikiwamo ukataji wa miti kwa ajili ya kuchana mbao.
Ametoa onyo hilo kufuatia tukio la kukamatwa kwa watu wawili, Guyashi Njile na Kelvin January, na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini Maswa (Mauwasa), wakidaiwa kukata miti katika eneo la chanzo cha maji la Madeco Farm, linalotumika kuhudumia wakazi wa Mji wa Maswa.
Akizungumza leo Jumatatu, Januari 5, 2026, Dk Anney amesema kufanya shughuli zozote za kibinadamu katika maeneo ya vyanzo vya maji ambayo yanalindwa kisheria ni kosa la jinai, na wote wanaokamatwa sheria itachukua mkondo wake.
Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk Vicent Anney. Picha na Maktaba
“Sheria itachukua mkondo wake bila kumuonea mtu yeyote. Hatutaruhusu uvamizi au shughuli zozote haramu katika vyanzo vya maji kwa sababu maji ni uhai wa wananchi,” amesema.
Dk Anney amesema uongozi wa Serikali wa wilaya hiyo, kwa kushirikiana na Mauwasa, utaendelea kufanya operesheni na doria za mara kwa mara ili kudhibiti uharibifu wa mazingira katika vyanzo vya maji.
Awali, akizungumzia hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mauwasa, Mhandisi Nandi Mathias, amesema uharibifu wa mazingira katika vyanzo vya maji una athari kubwa katika uendelezaji na uendelevu wa vyanzo hivyo.
“Ukataji miti katika vyanzo vya maji unasababisha kupungua kwa maji, kuharibu mazingira asilia na kuongeza gharama za uzalishaji wa maji safi na salama kwa wananchi,” amesema.
Mhandisi Nandi amesema Mauwasa haitaendelea kuvumilia vitendo hivyo na itaendelea kushirikiana na vyombo vya dola pamoja na wananchi kulinda vyanzo vyote vya maji vilivyopo chini ya mamlaka hiyo.
Baadhi ya mbao ambazo zimecharangwa zikiwa katika hifadhi ya Madeco Farm ambacho ni chanzo cha maji cha Mauwasa. Picha na Samwel Mwanga
John Magesa, mkazi wa Binza mjini Maswa, amesema vitendo vya uharibifu wa mazingira vimekuwa chanzo cha upungufu wa maji katika baadhi ya maeneo.
“Ni hatua ya kupongezwa. Vyanzo vya maji vikiharibiwa, sisi wananchi tunaumia moja kwa moja. Serikali iendelee kuchukua hatua kali,” amesema.
Naye Neema Magembe, mkazi wa Sola mjini Maswa, amesema maji ni uhai, hivyo watu wachache hawapaswi kupewa nafasi ya kuharibu mazingira katika vyanzo vya maji.
“Maji ni uhai. Watu wachache wasipewe nafasi ya kuharibu chanzo cha maji kinachohudumia jamii nzima,” amesema.
Watuhumiwa waliokamatwa wamekabidhiwa kwa vyombo vya dola kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.