Delcy Rodriguez: Mwanamke aliyetwaa madaraka katikati ya dhoruba ya kimataifa

Katikati ya usiku mzito wa Januari 3, 2026, Venezuela iliingia katika ukurasa mpya wa historia yake, ukurasa ulioandikwa si kwa kura, bali kwa helikopta, makombora na operesheni ya kijeshi ya kimataifa.

Nicolas Maduro, rais aliyeshikilia madaraka kwa mkono wa chuma alitekwa na kukamatwa na Marekani katika operesheni ya ghafla jijini Caracas. Ndani ya saa chache, swali kubwa likazuka: nani anashika hatamu za dola?

Jibu lilikuja haraka, lakini halikuwa rahisi. Delcy Eloina Rodriguez Gomez, Makamu wa Rais, Mwanasheria, Mwanadiplomasia mkongwe na mmoja wa watu waliokuwa karibu zaidi na Maduro alijikuta amesimama juu ya kilele cha mamlaka ya dola, si kwa uchaguzi, bali kwa mantiki ya kikatiba na uamuzi wa Mahakama ya Juu ya Venezuela.

Kuibuka kwa Delcy katika mazingira ya taharuki

Mahakama Kuu ya Venezuela ikiungwa mkono na jeshi, ilitoa uamuzi wa haraka: Delcy Rodriguez, Makamu wa Rais tangu mwaka 2018, achukue nafasi ya Rais wa Mpito.

Uamuzi huo haukuwa tu wa kikatiba; ulikuwa wa kisiasa, wa kimkakati na wa kulinda uhai wa dola ya Venezuela.

Ndani ya nchi, jeshi lilisimama upande wake. Nje ya nchi, Marekani ilimtazama kwa jicho la mashaka na matarajio kwa wakati mmoja.

Hapa ndipo simulizi ya Delcy Rodriguez inapogeuka kutoka kuwa hadithi ya mwanasiasa mkongwe wa mapinduzi ya Chavista na kuwa simulizi ya mwanamke aliyekalia kiti cha uongozi katikati ya mvutano wa kimataifa.

Kuibuka kwake kama Rais wa Mpito kulikuja na mkanganyiko wa papo hapo. Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza hadharani kuwa mawasiliano tayari yalikuwa yamefanyika kati ya Delcy na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio akidai kuwa Delcy alikuwa tayari kushirikiana na Washington.

Delcy Rodriguez hakutokea katika siasa kama bahati au ajali. Alizaliwa Mei 18, 1969 katika familia iliyogubikwa na siasa, mapambano na damu.

Baba yake, Jorge Antonio Rodriguez alikuwa mwanzilishi wa Socialist League, chama cha mrengo wa kushoto chenye misimamo mikali.

Alikamatwa mwaka 1976 kwa tuhuma za kuhusika katika utekaji wa mfanyabiashara Mmarekani William Niehous, na baadaye alifariki akiwa kizuizini, akidaiwa kuteswa na vyombo vya dola.

Kifo hicho kilikuwa alama ya kudumu katika maisha ya Delcy Rodríguez. Kilimjengea mtazamo wa dunia uliojaa mashaka kwa Marekani, chuki dhidi ya uingiliaji wa kigeni, na utii kwa itikadi ya mapinduzi ya kijamii.

Elimu, umahiri na tabia isiyopinda

Delcy alisomea sheria katika Chuo Kikuu Kikuu cha Venezuela (UCV), kisha akaendeleza masomo ya sheria za kazi huko Paris Ufaransa. Akiwa mwanafunzi alijitokeza kama kiongozi mwenye msimamo, asiyeogopa mamlaka. Tabia hiyo ilimfuata hadi katika ngazi za juu za serikali wakati mwingine ikimletea sifa, wakati mwingine migogoro.

Katika utumishi wake wa awali chini ya Rais Hugo Chavez, Delcy alijulikana kwa kutofuata heshima za kiserikali zilizojengwa juu ya unyenyekevu wa kisiasa.

Ripoti kadhaa zilieleza migongano yake na Chavez mwenyewe, hali iliyomfanya kwa muda kujiondoa katika mduara wa karibu wa mamlaka. Lakini hakuwahi kuondoka kwenye mfumo.

Umaarufu wake mkubwa ulijengwa alipoteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje mwaka 2014, akiwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo katika historia ya Venezuela.

Ndani ya muda mfupi, Delcy alijijengea taswira ya balozi mkali, asiyeogopa lugha nzito, mashambulizi ya moja kwa moja, wala majukwaa ya kimataifa.

Katika mikutano ya Mercosur, OAS (Jumuiya ya Nchi za Amerika) na Umoja wa Mataifa, alisimama kama ngao ya serikali ya Maduro. Alipambana na viongozi wa Argentina, Peru, na Katibu Mkuu wa OAS, Luis Almagro, akiwaita wavamizi, wanafiki na vibaraka wa maslahi ya kibeberu.

Lugha yake ilikuwa kali, lakini iliwafurahisha wafuasi wa Chavismo (itikadi ya kisiasa na harakati ya kijamii iliyoanzishwa na Hugo Chaves) ndani ya Venezuela.

Alipoteuliwa kuwa Makamu wa Rais mwaka 2018, Delcy alikabidhiwa si tu ofisi ya kisiasa, bali pia udhibiti wa vyombo nyeti vya dola, ikiweamo huduma ya ujasusi (SEBIN) na usimamizi wa uchumi uliokuwa umeparaganyika kwa mfumuko wa bei na vikwazo vya kimataifa.

Kwa mshangao wa wengi, alifanikiwa kuleta utulivu wa taratibu katika uchumi wa Venezuela na kuongeza uzalishaji wa mafuta licha ya vikwazo vikali vya Marekani.

Alijenga mawasiliano ya kimyakimya na wafanyabiashara wa kimataifa, wakiwamo baadhi ya Wa- Republican wa sekta ya mafuta waliokuwa wanapinga mabadiliko ya utawala kwa nguvu.

Januari 3, 2026: Siku ambayo historia ilipinduliwa

Operesheni ya Marekani ya kumkamata Rais Maduro ilikuwa tukio lililovunja kanuni zote za kawaida za diplomasia.

Ndani ya Venezuela lilitafsiriwa kama uvamizi. Nje, lilitangazwa kama hatua ya lazima. Ndani ya ombwe hilo, Delcy alisimama.

Awali, alidai uthibitisho kuwa Maduro alikuwa hai. Kisha, kupitia Mahakama Kuu, alipewa mamlaka ya Rais wa Mpito. Marekani ilidai kuwa alikuwa tayari kushirikiana, huku Rais Donald Trump akimtishia waziwazi endapo hatatii masharti ya Washington.

Lakini katika hotuba yake ya kwanza kwa taifa, Delcy hakuyumba. Alimtaja Maduro kama “Rais halali wa Venezuela,” akaapa kuwa nchi yake haitakuwa koloni la taifa lolote na akalaani kitendo cha Marekani kama uhalifu dhidi ya sheria za kimataifa.

Ndani ya saa 24, ulimwengu ulimwona Delcy katika sura mbili; mwanamapinduzi mkali kwenye televisheni ya taifa na mwanadiplomasia mpole kwenye ujumbe wa Instagram akizungumza kuhusu “ushirikiano wa heshima” na Marekani.

Mabadiliko hayo hayakuwa udhaifu, yalikuwa mkakati. Delcy alijua kuwa kuokoa dola ya Venezuela kulihitaji si misimamo migumu pekee, bali pia busara ya kisiasa.

Kikatiba, nafasi yake ni ya muda. Lakini Mahakama Kuu haikutaja kikomo cha siku 180. Wachambuzi wengi wanaamini Delcy Rodríguez anaweza kujaribu kubaki madarakani zaidi ya muda uliotarajiwa, akijenga muafaka ndani ya chama cha kijamaa, jeshi na sekta ya uchumi, wakati akijikinga dhidi ya uchaguzi mgumu.

Delcy si rais wa kawaida, wala si mpito wa kawaida. Yeye ni zao la historia ya mapambano, majeraha ya kisiasa na ulimwengu unaogombania rasilimali za Venezuela. Anaungwa mkono na jeshi, anapingwa na Marekani, anaheshimiwa na wafuasi wa Chavismo, na anachunguzwa kwa karibu na ulimwengu.

Katika saa hii ya giza la kitaifa, Delcy Rodriguez amekuwa uso wa uthabiti au labda wa mpito kuelekea mgogoro mkubwa zaidi.

Historia bado inaandika hukumu yake. Lakini jambo moja ni hakika: jina lake tayari limechongwa katika kurasa nzito za historia ya Venezuela.