Unguja. Serikali imesema itaendelea kuwekeza katika elimu inayojenga umahiri, ujuzi na maadili kwa lengo la kukabiliana na maisha pamoja na soko la ajira.
Azma hiyo ya Serikali imeelezwa leo, Jumatatu Januari 5, 2025, na Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, katika hafla ya ufunguzi wa shule ya sekondari ya Chukwani, kwa niaba ya shule ya Regezamwendo na Maungani, Mkoa wa Mjini Magharibi, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Amesema, kwa mazingira yanayotengenezwa na Serikali, uwezo wa kuandaa vijana wenye sifa hizo upo bila hofu wala tatizo lolote kwa sababu walimu wapo na wanafunzi wanapaswa kufanyia kazi.
Pia amesema Serikali itahakikisha inajenga shule za kisasa zinazoendana na mtaala mpya wa elimu, kwa lengo la kuleta tija halisi kama ilivyokusudiwa.
“Serikali zote mbili zitashirikiana kuhakikisha mipango inayopangwa inatekelezeka kwa manufaa ya wananchi wote,” amesema.
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba akifungua Shule ya Sekondari Chukwani, Zanzibar. Leo Januari 05, 2026 ikiwa ni sehemu ya shamrashamra ya maadhimisho ya Miaka 62 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Picha na Mtandao
Hivyo, ametoa wito kwa wananchi kuitunza miundombinu hiyo, kwani Serikali ni waratibu wa miradi hiyo iliyowekezwa kwa gharama kubwa, na wao wanapaswa kuilinda na kuitunza kwani hiyo ni mali yao.
Amesema waliozaliwa kabla ya Mapinduzi walisoma kwenye majengo ambayo hayakutosheleza, ila wanafunzi wa sasa wamepata kusoma kwenye majengo ya kisasa na yenye hadhi.
Amesema miundombinu hiyo inadhihirisha Mapinduzi kwa vitendo juu ya uimarishaji wa utoaji huduma za kijamii na kukidhi mahitaji ya mtaala.
Ameeleza kuwa elimu imekuwa chombo cha msingi wanachokitumia kuimarisha maisha yao na kufungua fursa za kiuchumi na kijamii katika ujenzi wa Taifa.
Amesema elimu ndio urithi pekee kwa vizazi vya sasa na vijavyo, hivyo wanafunzi wanapaswa kutoa zawadi ya kuelewa masomo yao na kuyafanyia kazi ipasavyo.
Mwonekano wa jengo la Shule ya Sekondari Chukwani, Zanzibar ambayo imefunguliwa leo Januari 5, 2025 na Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba. Picha na Mtandao
Hata hivyo, ametoa wito kwa jamii kuendelea kuitunza amani kwa lengo la kupata maendeleo ya nchi.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Khamis Abdulla Said, amesema ujenzi wa shule hizo umegharimu Sh.6.1 bilioni na inachukua wanafunzi 1,890, kwa wastani wa wanafunzi 45 kila darasa.
Amesema awali shule hiyo ilichukua wanafunzi 2,000, kwa wastani wa wanafunzi 100 kila darasa, hivyo ujenzi huo umesaidia kupunguza msongamano kwenye madarasa.
Pia, Katibu Khamis amesema wizara hiyo inandaa vijana kuwa wabunifu kwa kuweza kuyatumia mafunzo wanayopata shule katika maisha yao.
Kwa upande wake, Naibu wa Wizara hiyo, Khadija Salum Ali, amesema wizara itaendelea kusimamia elimu visiwani hapa ili wanafunzi wapate elimu bora.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Hamad Masauni, amesema Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, ana kazi kubwa na nzuri ya kuleta mabadiliko visiwani hapa.
Waziri huyo amesema watapita kila wilaya na mkoa kutoa elimu ya Muungano ili kusambaza elimu hiyo kwa wananchi.
