VIJANA nchini Kenya wamewapongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya Kenya, Mheshimiwa Dkt. William Samoei Ruto kwa uongozi wao thabiti na juhudi kubwa wanazoendelea kuzionesha katika kuwatumikia wananchi wao, licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali za kisiasa, kiuchumi na kijamii katika nyakati tofauti.
Pongezi hizo zilitolewa jijini Nairobi, kando ya Bunge la Wananchi, wakati vijana hao walipokuwa wakizungumza na Mwinjilisti na Muhubiri wa Kimataifa kutoka Tanzania, Dkt. Alphonce Boniface Temba.
Dkt.Temba, ambaye alifika nchini Kenya kwa ajili ya kutoa huduma ya injili, alitumia pia fursa hiyo kushiriki katika mijadala ya kijamii ndani ya Bunge hilo, ambapo aliwahutubia vijana na kuwapa neno la faraja, matumaini na mshikamano wa kikanda.
Katika hotuba yake, Dkt.Temba aliwahimiza vijana wa Kenya na Tanzania kutambua kuwa mataifa hayo mawili ni ndugu wa karibu kihistoria, kiutamaduni na kijiografia, na kwamba hakuna nguvu inayopaswa kuwatenganisha.
Pia, alisisitiza umuhimu wa kudumisha mshikamano na umoja wa kikanda kwa maslahi mapana ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kwa upande wao, vijana hao waliwashauri viongozi wa mataifa hayo mawili kuangalia kwa kina uwezekano wa kubadilisha mfumo wa uendeshaji wa shughuli za kiuchumi ili ziwe zinafanyika kwa saa 24.
Kwa mujibu wa vijana hao, utekelezaji wa mfumo huo utakuwa chachu muhimu ya kukuza uchumi, kuongeza tija na kutoa fursa pana zaidi za maendeleo kwa wananchi, hususan vijana.
Walieleza kuwa,tayari kuna jitihada zinazoonekana katika baadhi ya mataifa ya Afrika Mashariki, ikiwemo Tanzania hususan katika sekta ya usafirishaji na utoaji wa huduma muhimu kwa saa 24.
Hatua hiyo, walisema, imeendelea kulifanya Taifa la Tanzania kuwa mfano wa kuigwa katika kuonesha mwelekeo sahihi wa uendeshaji wa shughuli za kiuchumi zenye tija.
Vijana hao walifafanua kuwa,mfumo wa uchumi wa saa 24 utawawezesha wananchi kufanya kazi kwa mfumo wa mzunguko (shift system), ambapo wale wa zamu ya mchana watapumzika baada ya kazi na kuwaachia wale wa zamu ya usiku kuendelea na uzalishaji.
Mfumo huo, kwa maelezo yao, hautaongeza tu ajira, bali pia utaongeza uzalishaji wa bidhaa na huduma, hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi na ustawi wa jamii kwa ujumla.
Kwa upande mwingine, ilielezwa kuwa haikuwa rahisi kwa Dkt. Temba kukubalika mara moja ndani ya Bunge la Kijamii la Wakenya, kutokana na kuwepo kwa hisia na mitazamo hasi iliyokuwa imejengeka miongoni mwa baadhi ya wananchi wa Kenya kuhusu uongozi wa Tanzania.
Baadhi ya mitazamo hiyo, ilidaiwa kuwa, ilitokana na taarifa potofu zilizodai kuwa viongozi wa Tanzania walikuwa wakikandamiza upinzani na kuwaonea wananchi.
Hata hivyo, kupitia maelezo ya kina yaliyochukua takribani dakika 45, Dkt.Temba aliweza kufafanua hali halisi ya maisha ya wananchi wa Tanzania, mazingira ya kisiasa pamoja na msimamo wa vyama vya upinzani, ikiwemo hatua ya baadhi yao kuandika barua na kutoa taarifa kwa vyombo vya habari zikieleza kutoshiriki katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Alieleza kuwa, uchaguzi huo ulifanyika kwa kuzingatia taratibu zilizopo na kwamba, kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), alipata ushindi wa kura nyingi na wa kishindo, hali iliyodhihirisha imani ya wananchi kwa uongozi wake.
Kutokana na maelezo hayo, Dkt.Temba aliwataka wananchi wa Kenya kuachana na maneno na taarifa alizozitaja kuwa zimetengenezwa na maadui wa maendeleo, akisisitiza kuwa maneno hayo hayaliletei Taifa afya na wala hayachangii kuimarisha umoja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Baada ya kuwasilishwa kwa hoja hizo nzito na za kina, wajumbe wa Bunge la Wananchi walikubaliana kwa kauli moja na kutoa pongezi kwa Rais wa Kenya, Mheshimiwa Dkt. William Ruto, na Rais wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zao za kuongoza mataifa yao katika misingi ya kazi, uthubutu na uzalendo.
Aidha, waliendelea kuwaomba viongozi wa Afrika Mashariki kuwaangalia vijana kwa jicho la pekee, hususan katika nyanja za kiuchumi, ili kuwapatia fursa zitakazowawezesha kujikwamua kimaisha.
Kwa mujibu wa vijana hao, Afrika Mashariki ina rasilimali na fursa nyingi ambazo, iwapo zitatumika ipasavyo, zinaweza kuwainua vijana kiuchumi na kulisukuma eneo hilo kuelekea maendeleo ya haraka na endelevu.
Awali, mwandishi wa habari hizi ambaye alifuatilia kwa karibu mkutano huo alifanikiwa kuwapata Wakenya wawili kwa mahojiano maalum.
Wakenya hao ni James Mongi mkazi wa Mtaa wa Gaborone jijini Nairobi na Mussa Abdallah Rashid mkazi wa Mombasa na mfanyabiashara ndogo ndogo anayechukua biashara Nairobi kupeleka Mombasa.
Katika mazungumzo hayo, James Mongi amesema kuwa, kazi aliyoifanya Dkt.Alphonce Boniface Temba ni kazi iliyotukuka na ilipaswa kufanywa na Balozi wa Tanzania.
Mongi amesema, Wakenya wengi walikuwa hawana taarifa za ndani na ukweli kuhusu nini kinachoendelea, lakini ghafla Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye alikuwa kipenzi chao, wakajikuta wamejengewa chuki na kumchukia huku wakimtukana.
Aidha, Mongi kwa niaba ya vijana wa Kenya alimuomba Rais Dkt.Samia msamaha kwani haikuwa dhamira yao na wengi ni vijana wadogo wasiojitambua.
Aidha, wamesema walikorogwa Kenya na Tanzania kutokana na taarifa potofu ambazo walikuwa wanazipata Club House, Marekani, Japan na kwingineko.
Vilevile, amesema taarifa potofu kuhusu Tanzania walikuwa wanazipata kwa baadhi ya wanaharakati ambao wamejificha nchini humo bila kuwataja majina yao.
Amesema, kutokana na kupandikizwa taarifa potofu kuhusu Rais Samia walijikuta wanamchukia, hivyo kutumia kila namna kumchafua.
Aidha, wamemuoba Rais Dkt.Samia kuwasamehe kwani, Tanzania ni kama nyumbani na wanafanya biashara, wanavuka mipaka kuja kutibiwa huku Watanzania nao wakivuka kufanya biashara na hata kupata huduma za matibabu.
“Hivyo, sisi Wakenya na Watanzania ni ndugu wa damu, mwambie Mheshimiwa Rais Dkt.Samia, sisi watoto wake hapa Kenya tunampenda na tunaomba msamaha kwake.”
Kwa upande wake, Abdallah amefurahi kupata ukweli kuhusu Tanzania kupitia Dkt.Temba hususani uhuru wa wapinzani nchini Tanzania.
Amesema,vijana wa Kenya wamegundua kuwa wapinzani waliandika barua hasa CHADEMA kupitia Katibu Mkuu, John Mnyika na akatoka hadharani kueleza kuwa, hawatashiriki uchaguzi.
Amesema, CHADEMA ilionesha udhaifu mkubwa kwani walipaswa kushiriki uchaguzi huo ili kuweza kushughulikia madhaifu waliyodai yapo wakiwa majukwaani na si kususa.