HATUWADAI: Taifa Stars ilivyoaga AFCON kwa heshima

TAIFA Stars imehitimisha safari yake ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) katika hatua ya 16-Bora baada ya kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya timu Na.1 kwa ubora wa barani Afrika, Morocco katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Prince Moulay Abdellah mbele ya maelfu ya mashabiki waliofurika.

Matokeo hayo, ingawa yanaumiza, hayaondoi ukweli kuwa Tanzania imeondoka Morocco kifua mbele, ikionyesha kuwa sio timu ya kushiriki tu bali ni shindani kutokana na kiwango kilichoonyeshwa dhidi ya vigogo wa soka la Afrika kuanzia hatua ya makundi hadi mtoano.

Morocco iliingia uwanjani kama moja ya timu zinazopewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa, lakini Taifa Stars ilionyesha nidhamu ya hali ya juu chini ya kocha Miguel Gamondi. Licha ya Morocco kumiliki mpira kwa muda mrefu, muundo wa kujilinda kwa Tanzania ulikuwa imara na uliwazuia kupata nafasi nyingi za wazi.

Katika mechi hiyo, Gamondi aliamua kutumia mabeki watatu wa kati, Bakari Mwamnyeto, Dickson Job na Ibrahim Hamad Bacca huku wakisaidiwa na Mohammed Hussein na Haji Mnoga kama mawing-backs.

Simon Msuva alikosa bao la wazi katika lango tupu aliposhindwa kuunganisha kwa kichwa krosi tamu ya Selemani Mwalimu ‘Gomez’ iliyopita juu ya kipa na kumkuta straika huyo jirani na nguzo ya mbali, lakini akapiga kichwa nje.

Morocco walifunga bao katika dakika ya 15 lililodhaniwa kuwa ni la kuongoza, kupitia Ismael Saibari, lakini VAR ilibaini kwamba nyota huyo aliotea. Tukio hilo liliwapa nguvu Taifa Stars, ambao waliendelea kutekeleza mpango kazi wao vizuri.

STA 02

Mbali na Msuva, Tanzania ilipata nafasi nyingine kadhaa za kufunga ikiwamo ya Feisal Salum aliyepaisha mpira aliosetiwa vyema na Gomez. Dhidi ya timu yenye ubora kama Morocco, makosa madogo kama haya huwa na gharama kubwa.

Hatimaye, bao pekee la mchezo lilifungwa katika dk64 na nyota wa Real Madrid, Brahim Diaz, aliyefanya kazi kubwa binafsi kabla ya kufunga, akisaidiwa na Achraf Hakimi. Bao hilo ndilo lililotenganisha timu hizo mbili, si kwa sababu Tanzania ilikuwa dhaifu, bali kwa sababu Morocco ilitumia vizuri nafasi hiyo.

STA 04

Dakika za mwisho za mchezo ndizo zilizoacha maswali mengi mioyoni mwa Watanzania. Katika muda wa nyongeza, Iddi Nado ambaye aliingia dk83 kuchukua nafasi ya Alphonce Mabula aliangushwa ndani ya eneo la hatari la Morocco. Wachezaji wa Stars walishinikiza madai ya penalti, lakini mwamuzi wa kati Dahane Beida alipuuza kilio cha Taifa Stars.

Uamuzi huo uliibua hasira na masikitiko makubwa kwa wachezaji, benchi la ufundi na mashabiki, wakiamini kuwa Tanzania ilinyimwa haki ya kupata penalti ya wazi, ambayo ingeweza kuisawazishia timu na kupeleka mchezo muda wa ziada.

Ingawa safari ya AFCON hii imefikia mwisho, safari kubwa zaidi ndiyo inaanza sasa. Tanzania ni mwenyeji mwenza wa AFCON 2027 pamoja na Kenya na Uganda, jambo linalobeba matumaini makubwa kwa taifa. Hii ni nafasi nyingine ya Kihistoria.

Chini ya kocha Gamondi, Taifa Stars imeonyesha kuendelea kuwa katika mwelekeo sahihi baada ya kazi nzuri iliyofanywa na kocha Hemed Suleiman Morocco sambamba na Juma Mgunda na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’.

Kazi iliyopo sasa ni kuendelea kukijenga kikosi hicho.

STA 03

Gamondi, hakuificha hisia zake baada ya kuondolewa kwenye mashindano hayo, kocha huyo ameridhishwa na kiwango cha wachezaji, akisisitiza kuwa walitekeleza maelekezo ya kiufundi kwa nidhamu na ujasiri mkubwa.

“Ninajivunia sana wachezaji wangu. Walipambana, waliheshimu mpango wa mchezo na waliamini kuwa wanaweza kushindana na Morocco. Huu ni uthibitisho kuwa Taifa Stars inapiga hatua,” anasema Gamondi, ambaye ni kocha wa mpito Stars.

STA 01

Hata hivyo, kocha huyo raia wa Argentina hakusita kueleza masikitiko yake juu ya baadhi ya maamuzi ya waamuzi, hasa tukio la dakika za mwisho ambapo Tanzania ilidai penalti.

“Ni vigumu kukubali matokeo kama haya pale unapohisi kuna uamuzi ambao ungebadilisha hatima ya mchezo. Tuliona tukio lililostahili kuangaliwa kwa makini zaidi. Huo ni uamuzi unaoumiza, hasa katika mchezo wa aina hii,” anaongeza.

Gamondi anasema kuwa, licha ya maumivu ya kuondolewa, uzoefu walioupata wachezaji wake ni mtaji mkubwa kuelekea mashindano yajayo, hususani maandalizi ya muda mrefu ya AFCON 2027 ambayo Tanzania itakuwa mwenyeji mwenza pamoja na Kenya na Uganda.