Caracas. Ikiwa ni siku moja imepita tangu vikosi vya Marekani kumkamata Rais Nicolas Maduro, Serikali ya Venezuela imetoa ujumbe kwa jumuiya ya kimataifa na hasa kwa Marekani, ikisisitiza dhamira yake ya kudumisha amani, kuishi kwa kuheshimiana na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa bila vitisho.
Katika taarifa iliyochapishwa katika mitandao ya kijamii leo Jumatatu Januari 5, 2026 na rais wa mpito wa Venezuela, Delcy Rodríguez, amesema taifa hilo linaamini kuwa amani ya dunia hujengwa kwa kuhakikisha kwanza amani ndani ya kila nchi.
“Hii ndiyo Venezuela ninayoamini ambayo nimeitolea maisha yangu. Nina ndoto ya kuona Wavenezuela wote wema wakija pamoja kwa ajili ya taifa lao,” amesema.
Rodríguez amesema serikali yake inatoa kipaumbele katika juhudi za kuweka uhusiano wa usawa na wenye kuheshimiana kati ya Venezuela na Marekani, pamoja na mataifa mengine ya ukanda huo, kwa misingi ya usawa wa mamlaka ya mataifa na kutoingiliwa kwa masuala ya ndani.
Aidha, ametoa wito kwa Marekani kufanya mazungumzo ya amani katika ajenda ya maendeleo ya pamoja.
“Tunaialika serikali ya Marekani kushirikiana na sisi katika ajenda ya ushirikiano unaolenga maendeleo ya pamoja ndani ya mfumo wa sheria za kimataifa, ili kuimarisha kuishi kwa amani kwa jamii zetu,” amesema Rodriguez.
Rodríguez alimrejea Rais wa Marekani, Donald Trump, akisema yeye, wananchi wa Venezuela na ukanda mzima wanastahili amani na mazungumzo badala ya vita.
“Rais Donald Trump, watu wetu na ukanda wetu wanastahili amani na mazungumzo, si vita. Huu umekuwa ujumbe wa Rais Nicolás Maduro wakati wote, na kwa sasa ni ujumbe wa Venezuela nzima,” amesema.
Rodriguez, ambaye pia ni Waziri wa Mafuta, amekuwa akitajwa kwa muda mrefu kuwa miongoni mwa viongozi wenye msimamo wa vitendo zaidi ndani ya serikali ya Maduro. Rais Trump aliwahi kusema anaamini Rodriguez yuko tayari kufanya kazi na Marekani.
Hata hivyo, Rodriguez na maofisa wengine wa serikali hiyo wameeleza kukamatwa kwa Maduro na mkewe, Cilia Flores, kuwa ni utekaji nyara, wakisisitiza kuwa Maduro bado ni kiongozi halali wa Venezuela.
Vilevile, Rais Maduro, anatarajiwa kufikishwa mbele ya Mahakama ya Shirikisho ya Marekani mjini New York leo, kufuatia kukamatwa kwake mwishoni mwa wiki katika oparesheni ya kijeshi iliyoendeshwa na majeshi ya Marekani mjini Caracas.
Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema kuwa Marekani itachukua hatua nyingine za kijeshi endapo Venezuela haitashirikiana na juhudi za Marekani kufungua sekta ya mafuta na kukabiliana na biashara ya dawa za kulevya.
