Januari hii ni zaidi ya ada, hadi vyakula vimepanda

Dar/mikoani. Ukiacha mzigo wa malipo ya ada za wanafunzi na gharama nyingine za maisha kila inapoanza Januari, mwaka huu hali imekuwa mbaya zaidi, kwani makali yamegusa hadi kwenye bei za vyakula.

Si unga wa mahindi wala mchele pekee, dagaa na viazi mviringo, vyote vimepanda bei ndani ya Januari, hasa katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Dodoma, Kilimanjaro na Mbeya, ambako Mwananchi imefanya uchunguzi.

Hali imekuwa hivyo wiki chache tangu Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, alipowahakikishia Watanzania kuwa hakutakuwa na upungufu wa chakula kwa kuwa nchi ina akiba ya kutosheleza miezi sita hata isipozalisha kabisa.

Hata hivyo, alisema mfumko wa bei unapotokea huwa na mambo mawili, ama hali halisi au hutengenezwa na watu.

Trey za mayai zikiwa dukani.

“Nikupe mfano, mimi ni mzalishaji wa sukari, nikiamua kutengeneza mfumko wa bei basi siitoi tu kwenye soko kwa wiki moja au mbili ili kuwe na uhaba, ila ukikamatwa wewe ni mhujumu uchumi,” alisema.

Wafanyabiashara wamesema ongezeko hilo la bei, limechochewa na mahitaji makubwa dhidi ya usambazaji wa bidhaa husika, huku baadhi ya wananchi wakiiomba Serikali kuchukua hatua za haraka kudhibiti hali hiyo, kuongeza usimamizi wa masoko, kuimarisha uzalishaji wa ndani na kulinda walaji dhidi ya kupanda kwa bei.

Kwa nyakati tofauti leo, Jumatatu Januari 5, 2026, baadhi ya wananchi wamesema hali hiyo inawalazimisha kuishi kwa kubadili ratiba ya chakula, kutozingatia ulaji wa milo mitatu.

“Kwangu, tukinywa chai saa 5 asubuhi basi tutakula tena saa 11 jioni ndiyo mpaka kesho yake. Siwezi kumudu tena milo mitatu kwa maana ya asubuhi, mchana na jioni,” amesema Kondo Mustapha wa Mabibo.

Mbali na baadhi ya familia kubadili ratiba ya chakula, hali si shwari pia kwa watu wanaokula kwa mama lishe, kwani nako bei imeongezeka kutoka sahani ya wali nyama au ugali na nyama Sh2,000 hadi Sh2,500.

Kwa wapenzi wa chipsi, nao bei imeongezeka kutoka Sh1,500 hadi Sh2,000 kwa chipsi kavu, na chipsi mayai ikiwa Sh3,000 kutoka Sh2,500 kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.

Bei ya chipsi haijawaumiza tu wakazi wa Dar es Salaam, kwani hata jijini Dodoma nako, tangu Januari mosi mwaka huu, bei ya chipsi mayai imepanda hadi Sh4,000 kutoka Sh3,000 iliyokuwa ikiuzwa awali, na chipsi kavu ikitoka Sh2,000 hadi Sh3,000.

Masokoni nako hali si shwari, kwani wanunuzi wa bidhaa wameendelea kulia na bei. Kwa Dar es Salaam, katika Soko la Mabibo, gunia la viazi linauzwa Sh120,000 kutoka Sh95,000 iliyokuwa ikiuzwa Novemba.

Kwa wauzaji wa rejareja, sado iliyokuwa ikiuzwa Sh3,500 sasa ni Sh6,000, wakati ndoo ndogo iliyokuwa ikiuzwa Sh8,000 hadi Sh10,000 hivi sasa inauzwa Sh15,000.

“Bei zimepanda kuanzia huko shambani, viazi havishikiki, ndiyo sababu gunia limefika Sh120,000,” amesema mmoja wa wafanyabiashara wa jumla wa viazi sokoni hapo, Elineema Mushi.

Bei ya viazi imepanda pia katika masoko yaliyopo jijini Mbeya kutoka Sh12,000 hadi Sh14,000 kwa ujazo wa plastiki ya lita 20, huku fungu moja likiuziwa kati ya Sh500 hadi Sh1,000.

Mfanyabiashara katika Soko la Mabatini, Rehema Mwanjonde, amesema sababu ni pamoja na changamoto za uzalishaji na mwingiliano wa wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali nchini, ambao hupandisha bei kwa wakulima shambani.

Kilio hicho kimesikika pia Arusha, ambapo Meneja wa Soko la Kilombero, Jeremia Katemi, amesema gunia la viazi limepanda kutoka Sh70,000 hadi Sh100,000, huku karoti zikiongezeka kutoka Sh70,000 hadi kufikia Sh150,000.

Hali hiyo inatajwa kuchangiwa na mfumo wa manunuzi uliopo kila mwisho wa mwaka, ambapo watu hununua vyakula kwa wingi, hali inayofanya vipungue sokoni wakati ambao baadhi ya wasambazaji bado wanaendelea kusherehekea sikukuu na hawajaanza kuingiza mizigo mipya sokoni.

“Hiyo ndiyo inayofanya bidhaa kupanda kwa sababu kidogo kilichopo hakikidhi mahitaji ya wengi. Mabadiliko ya tabianchi pia ni moja ya eneo ambalo limeathiri sana mikoa ya uzalishaji kutopata mvua kwa kiwango kinachotakiwa, ikiwa ingepata mvua mwezi kama huu, baadhi ya maeneo mahindi yangekuwa yanachomwa,” amesema mtaalamu wa uchumi, Profesa Aurelia Kamuzora.

Kauli yake iliungwa mkono na mfanyabiashara wa mazao ya nafaka katika Soko la Mawenzi mkoani Morogoro, Rajabu Bwakila, anayeeleza kuwa mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha mvua kubwa ni sababu nyingine.

Mvua zinapozidi katika maeneo ya uzalishaji, miundombinu ya barabara huharibika au bidhaa kuharibika.

“Mfano, nyanya ikiwa shambani haitaki kabisa maji, ikipata maji inaoza kuanzia mche hadi nyanya yenyewe, na hapo ndiyo zinapoanza kupungua sokoni na bei ndipo inapoanza kupanda,” amesema Bwakila.

Aidha, amesema mvua zinapoharibu miundombinu, gharama za usafirishaji huongezeka, hivyo wafanyabiashara hulazimika kupandisha bei ili kufidia gharama hizo.

Muuza duka la jumla eneo la Kihonda, Joseph Mugabo, amesema Januari bidhaa zimekuwa zikipanda kwa sababu ya uchache wake sokoni.

“Tumetoka kwenye sikukuu za Krismasi na Mwaka mpya, wananchi wamenunua bidhaa hizi kwa wingi, hivyo upo uwezekano wa bidhaa nyingine kupungua shambani.

“Januari ni msimu wa kilimo na si wa mavuno, hivyo wakulima bado wanaweka vyakula ndani kwa ajili ya akiba kwa sababu hawajui msimu huu wa kilimo utakuaje. Ninaamini ikifika Machi na Aprili vyakula vitashuka bei,” amesema.

Mbali na maeneo hayo, bidhaa nyingine za chakula kama mchele nazo zimeongezeka bei, ambapo katika masoko ya Ilala na Buguruni umefikia Sh3,400 kwa mchele wa daraja la kwanza na Sh3,000 kwa ule wa kawaida kutoka Sh2,800 na Sh2,400.

Katika Soko la Mabibo, bei ni nafuu kidogo kwani mchele uliuzwa Sh3,000 na Sh2,600 kwa ule wa kawaida, wakati bei ya maharagwe ikishuka hadi Sh2,800 kutoka Sh3,000.

Jijini Mbeya, bei ya dagaa imetoka Sh14,000 hadi Sh18,000 kwa sado moja, huku yai moja likitoka Sh250 hadi Sh400, na trei moja ikiuzwa kati ya Sh8,000 hadi Sh9,000.

Mayai hayo hayo kwa mkazi wa Simiyu atalazimika kuwa na Sh500 hadi Sh600 ili apate yai moja, ikiwa ni ongezeko kutoka Sh300 hadi Sh350 iliyokuwa ikiuzwa awali, huku mpenzi wa chipsi yai akilazimika kulipa Sh3,500 kutoka Sh3,000.

Akizungumza, Stiven Swai kutoka Soko Kuu la Moshi amesema ongezeko la bei ya mayai limetokana na upungufu wa mayai sokoni, hali inayosababishwa na wafugaji wengi kuacha ufugaji kutokana na gharama kubwa za chakula cha kuku.

Mkazi wa mtaa wa Nyunguu mjini Babati, Halima Hamis, amesema hivi sasa dagaa wa Kigoma wanauzwa sado moja Sh8,000 hadi Sh10,000 badala ya Sh6,000 ya awali.

Huko Dodoma, bei ya mchele nayo imepanda kutoka Sh2,600 hadi Sh3,000 na Sh3,200 kwa kilo, huku maharagwe yakipanda kutoka Sh2,600 hadi Sh3,600 kwa kilo, sado ya nyanya ikipanda kutoka Sh4,000 hadi Sh10,000, na sado ya vitunguu ikitoka Sh5,000 hadi Sh7,000.

Unga nao bei ipo juu, ambapo mkazi wa mji mdogo wa Mirerani Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Adolf Elias, amesema ongezeko la bei ya mahindi ndilo sababu.

“Kwa sasa debe moja lililokuwa Sh8,000 hadi Sh10,000 sasa limepanda hadi kati ya Sh18,000 hadi Sh19,000. Kilo ya unga wa dona ni Sh1,400 badala ya Sh1,000 au Sh900. Vitu vimepanda bei, hivyo gharama za maisha zimezidi,” amesema.

Imeandikwa na Hawa Mathias (Mbeya), Bertha Ismail (Arusha), Rachel Chibwete (Dodoma), Samwel Mwanga (Simiyu), Mariam Mbwana, Imani Makongoro (Dar), Florah Temba (Kilimanjaro) na Joseph Lyimo (Manyara).