Kanisa la TMC latoa mkono wa pole Mpwapwa

Mpwapwa. Kanisa la Tanzania Methodist (TMC) limetoa mkono wa pole kwa washirika wa kanisa hilo waliopata majanga ya nyumba zao kuezuliwa na mvua yenye upepo mkali iliyonyesha Desemba 18, 2025 wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma.

‎Kanisa hilo limetoa msaada wa vifaa vya ujenzi kama mabati, misumari na mbao, vyandarua 200 vyenye dawa ya kuua mbu na mahindi magunia saba.

‎Akizungumza wakati wa ibada ya Jumapili ya Januari 4, 2026 Askofu Mkuu wa TMC Samuel Nyanza amesema ni jukumu la kanisa kuihudumia jamii inayolizunguka hasa katika kipindi cha majanga.

‎Askofu Nyanza amesema tangu alipopata taarifa ya waumini hao kupata majanga ya kukosa makazi hakuweza kupata usingizi bali alikimbia huku na kule kuomba msaada ili waumini hao warudi kwenye maisha yao ya kawaida.

Mkazi wa kitongoji cha Visele A Kata ya Mazae Wilayani Mpwapwa, Erasto Masaluje akiangalia nyumba yake baada ya kuifanyia ukarabati kutokana na kuezuliwa na mvua yenye upepo iliyonyesha Desemba 18, 2025. Picha na Rachel Chibwete

‎”Nilipopata taarifa hizi sikulala, cha kwanza nilichofanya ni kuleta chakula kwanza ili watu wale na kupata nguvu maana tumepata taarifa kuwa kuna familia 20 za waumini wetu wanahitaji chakula kwa hiyo kanisa litawagawia kila familia debe mbili za mahindi kwa ajili ya chakula,” amesema Askofu Nyanza na kuongeza kuwa,

‎”Lakini kutokana na hali ya hewa iliyopo tutawagawia vyandarua vyenye dawa ya kuua mbu waenezao malaria ili kujikinga na magonjwa wakati kanisa linaangalia uharibifu uliofanyika ili tuweze kuwasaidia kurudi kwenye maisha yenu ya kila siku.”

‎Mmoja wa waathirika ambaye ni mkazi wa Kata ya Mazae Wilayani Mpwapwa, Erasto Masaluje amesema nyumba yake iliezuliwa paa.

‎Amesema nyumba hiyo inahitaji mabati mapya saba, mbao na misumari ili aweze kupaua upya huku akimshukuru Mungu kwa familia yake kutodhurika kutokana na kimbunga hicho.

‎Kwa upande wake Joyce Mchela amesema ili nyumba yake itengemae anahitaji mabati mapya nane kwani yale ya mwanzo yalisombwa na upepo.

Moja ya nyumba iliyoezuliwa na mvua yenye upepo Wilayani Mpwapwa, Desemba 18, 2025. Picha na Rachel Chibwete

‎Akizungumzia tukio hilo mchungaji wa kanisa hilo, Silvester Ngowo amesema baada ya kutokea kwa kimbunga hicho na waumini wa kanisa hilo kukosa makazi walitoa taarifa kwa askofu mkuu ambaye amefika na kuwasaidia.

‎Amesema mbali na waumini wa kanisa hilo kuna nyumba nyingine zaidi ya 100 ambazo ziliezuliwa na kimbunga eneo la Mazae wilayani Mpwapwa na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali.

‎Amelishukuru kanisa kwa kuwa msaada wakati wa majanga hayo kwani wengine walilazimika kuhamia kanisani baada ya kukosa makazi.

‎ Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mazae Kati, Abedinego Msanjila amesema mbali na nyumba kuezuliwa na kimbunga hicho, nyingi zilijaa maji na vyoo kubomoka.