Kikwete aridhishwa na miradi ya maendeleo Pemba

Pemba. Rais mstaafu, Jakaya Kikwete amesema ameridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kisiwani Pemba hatua iliyoimarisha utoaji wa huduma za kijamii, kukuza uchumi na kuongeza kipato cha wananchi.

Kikwete amesema hayo leo Jumatatu, Januari 5, 2026, alipozungumza na wananchi baada ya kuzindua Ofisi ya Uhamiaji Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Uzinduzi huo ni miongoni mwa shughuli za kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Rais Kikwete amesema Pemba imepata mabadiliko makubwa ya kimaendeleo ikilinganishwa na miaka iliyopita, hali inayotokana na kuimarishwa kwa miundombinu ya utoaji huduma.

Hivyo, amewahimiza wananchi kuendelea kuunga mkono Serikali zilizopo madarakani ili juhudi hizo ziendelee kuleta tija.

“Pemba ya sasa ni tofauti na ya zamani. Kwa kweli miradi mingi ya maendeleo imefanyika hapa. Hili ni jambo linalopaswa kuungwa mkono kwa kuendelea kuziunga mkono jitihada za viongozi waliopo madarakani,” amesema Kikwete.

Akizungumzia Ofisi ya Uhamiaji Micheweni, Kikwete amesema itaendeshwa kwa mifumo ya kidijitali, hatua itakayorahisisha na kuharakisha utoaji wa huduma kwa wananchi na wageni wanaohitaji huduma za uhamiaji.

“Nimeridhishwa na mabadiliko makubwa katika sekta mbalimbali. Uboreshaji wa barabara na bandari ni hatua muhimu inayochangia kukuza uchumi na kuifungua Pemba kiuchumi,” amesema.

Muonekano wa jengo la uhamiaji Micheweni Pemba.

Amesema ujenzi wa ofisi hiyo ni sehemu ya kuimarisha miundombinu rafiki inayokwenda sambamba na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amesema kuimarishwa kwa ofisi za uhamiaji kunachochea uwajibikaji na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Simbachawene amebainisha kuwa, Serikali imejipanga kuhakikisha watumishi wanapata makazi bora ili kuongeza motisha na ufanisi kazini.

Amesema Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa ofisi na makazi ya askari, hususan maeneo ya mipakani, kwa lengo la kuondoa changamoto za makazi na kuboresha usimamizi na udhibiti wa mipaka ya nchi.

Simbachawene amesema Idara ya Uhamiaji imepiga hatua kubwa kwa kuanzisha mifumo ya kielektroniki katika utoaji wa huduma Tanzania bara na Zanzibar.

Ametaja mifumo ya pasipoti za kielektroniki pamoja na mfumo wa uombaji na utoaji wa viza mtandaoni (Online Visa) kuwa imepunguza usumbufu kwa wageni na kuharakisha huduma wanapowasili nchini.

Amesema pia mfumo wa kielektroniki wa udhibiti na usimamizi wa mipaka umeanzishwa ili kuongeza ufanisi wa ulinzi na kuimarisha usalama wa nchi, huku ukiboresha udhibiti wa watu wanaoingia na kutoka pamoja na kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Awali akiwasilisha taarifa ya kitaalamu ya mradi huo, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Dk Islam Seif amesema ujenzi wa ofisi ya uhamiaji Micheweni umegharimu Sh2.549 bilioni.

Seif amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutenga fedha zitokanazo na mgao wa mapato ya Idara ya Uhamiaji  Zanzibar ili kutekeleza miradi ya kimkakati.

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Tanzania, Dk Anna Makakala ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikiano wake katika kuimarisha idara hiyo, akisema msaada wa maeneo na fedha kwa ajili ya ujenzi wa ofisi na makazi ya askari ni hatua ya kupongezwa.

Ameahidi kuwa, Idara ya Uhamiaji itatunza na kutumia majengo hayo kwa kuzingatia misingi na malengo yaliyokusudiwa.

Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mgeni Khatib Yahya amesema Serikali ya mkoa itaendelea kuwahamasisha wananchi kutumia ofisi hizo kupata huduma mbalimbali, zikiwamo huduma za pasipoti.