Kocha Dodoma Jiji aanika mipango yake

KOCHA wa Dodoma Jiji, Aman Josiah amesema timu itafanya mazoezi kwa wiki moja, huku ikiangalia ni mkoa gani ikienda itapata mechi za kirafiki kwa urahisi kabla ya kurejea mechi za ligi.

Ratiba inaonyesha Dodoma Jiji itakuwa wenyeji wa Tanzania Prisons katika mechi itakayopigwa Januari 22, jambo ambalo kocha huyo amesisitiza wanahitaji kupata pointi tatu, hivyo lazima wajipange.

“Tayari nimeupa uongozi programu ya mazoezi na mkoa ambao tunautarajia kama mambo yatakwenda sawa ni Manyara, Arusha, ambako tunaangalia zaidi uwezekano wa kupata timu ambazo tunaweza tukacheza nazo mechi za kirafiki,” amesema kocha huyo na kuongeza:

“Prisons ipo nafasi ya 13 na Dodoma nafasi ya 15 kila timu inahitaji pointi tatu hapo ili kuondoka nafasi mbaya katika msimamo wa Ligi Kuu, ndiyo maana lazima wachezaji wawe fiti kukabiliana na mechi hiyo.”

Amesema mbali na ugumu anaoutarajia kutoka kwa Prisons, msimu huu unahitaji mbinu zaidi ili kupata matokeo ya ushindi:

“Ukiangalia mechi nyingi zilizochezwa zimeamuliwa kwa mbinu kali, sina maana kwamba hakuna ufundi upo, lakini mbinu zinatawala zaidi.”