Maduro kufikishwa mahakamani Marekani leo

Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro, anatarajiwa kufikishwa mahakamani nchini Marekani leo baada ya kukamatwa mwishoni mwa wiki na vikosi vya Marekani, huku Rais wa Marekani, Donald Trump, akiweka wazi uwezekano wa uvamizi mwingine iwapo Marekani haitapata inachokitaka kutoka kwa kiongozi wa mpito wa nchi hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Jumapili, Trump alisema anaweza kuamuru shambulio jingine endapo Venezuela haitashirikiana na jitihada za Marekani kufungua sekta ya mafuta ya nchi hiyo na kukomesha biashara ya dawa za kulevya.

Pia alitishia kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Colombia na Mexico, na kusema kuwa utawala wa kikomunisti wa Cuba “unaonekana kuwa tayari kuanguka wenyewe.”

Balozi za Colombia na wa Mexico mjini Washington, zilipoombwa na waandishi wa habari kutoa maoni, hazikutoa majibu mara moja kutokana na kauli ya Trump.

Kauli za Trump zilitolewa siku moja kabla ya Maduro kupangwa kufikishwa mbele ya Mahakama ya Shirikisho mjini New York leo.

Maduro alikamatwa wakati wa uvamizi wa kijeshi uliofanyika Jumamosi mjini Caracas, tukio lililozua hofu kimataifa na kulizamisha taifa la Venezuela katika hali ya sintofahamu.

Maofisa wa serikali ya Trump wameeleza kukamatwa huko kama hatua ya utekelezaji wa sheria inayolenga kumwajibisha Maduro kwa mashtaka ya jinai yaliyofunguliwa mwaka 2020, yakimshutumu kwa kula njama ya ugaidi unaohusisha dawa za kulevya.

Hata hivyo, Trump mwenyewe amesema kulikuwa na sababu nyingine pia, akieleza kuwa uvamizi huo ulichochewa kwa sehemu na ongezeko la wahamiaji kutoka Venezuela wanaoingia Marekani, pamoja na uamuzi wa nchi hiyo wa kutaifisha maslahi ya mafuta ya Marekani miongo kadhaa iliyopita.

“Tunarejesha walichokiiba,” alisema jana akiwa ndani ya ndege ya Rais wa Marekani, Air Force One, alipokuwa akirejea Washington akitokea Florida. “Sisi ndio wenye mamlaka.”

Trump alisema makampuni ya mafuta yatarejea Venezuela na kujenga upya sekta ya mafuta ya nchi hiyo. “Watatumia mabilioni ya dola, na watatoa mafuta ardhini,” alisema.