Dar es Salaam. Mashahidi 117 wanatarajiwa kutoa ushahidi wao mahakamani katika kesi ya kuendesha biashara ya upatu inayomkabili Mkurugenzi wa Kampuni ya Vanilla International Ltd, Simon Mkondya, maarufu Dk Manguruwe, na mwenzake.
Pia, upande wa Jamhuri unatarajia kuwa na vielelezo zaidi ya 100. Mkondya na mwenzake, Rweyemamu John, ambaye ni meneja na mkaguzi wa fedha wa kampuni hiyo, wanakabiliwa na mashtaka 126 yakiwemo ya kuendesha biashara ya upatu na utakatishaji fedha, yanalomkabili Mkondya pekee.
John, yeye yupo nje kwa dhamana baada ya kuiomba dhamana Mahakama Kuu na hana mashtaka ya kutakatisha fedha.
Mashahidi hao wanatarajia kutoa ushahidi wao katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kuwasilisha kibali cha kuruhusu mahakama hiyo kusikiliza kesi hiyo ya uhujumu uchumi.
Hatua hiyo inatokana na upelelezi wa kesi hiyo kukamilika katika Mahakama ya mkoa wa Dar es Salaam.
Haya yameelezwa na Wakili wa Serikali, Titus Aron, leo Jumatatu, Januari 5, 2026, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya Jamhuri kuwasomea hoja za awali (PH) kwa washtakiwa hao.
Wakili Aron ametoa taarifa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki, anayesikiliza kesi hiyo.
Asomewa mashtaka mengine 126:
Kabla ya kusomewa PH, wakili wa Serikali aliwasomea upya mashtaka yao, ikiwemo kufanya mabadiliko ya hati ya mashtaka kwa kuongeza mashtaka kutoka 28 yaliyokuwepo awali hadi kufikia mashtaka 126.
Baada ya kubadilisha hati ya mashtaka, aliwasomea upya mashtaka yao na kisha kuwasomea hoja za awali.
Katika mashtaka hayo 126, mashtaka 117 ni ya kuendesha biashara ya upatu yanayowakabili washtakiwa wote wawili, na mashtaka tisani ya kutakatisha fedha yanayomkabili Mkondya pekee.
Katika moja ya mashtaka hayo ya kuendesha biashara ya upatu, washtakiwa wanadaiwa, kati ya Januari mosi 2020 na Desemba mosi 2023, jijini Dar es Salaam, kutenda makosa hayo.
Inadaiwa Mkondya akiwa kama Mkurugenzi wa kampuni hiyo, na John akiwa Meneja wake, waliendesha biashara ya upatu kwa kuwaahidi watu kupata faida mara mbili hadi tatu ya pesa walizotoa. Washtakiwa hao wanadaiwa kuijipatia pesa kutoka kwa watu zaidi ya 117, ambao walitoa kiasi tofauti cha fedha kwa kuwaahidi faida mara mbili hadi tatu.
Katika mashtaka tisa ya utakatishaji fedha yanayomkabili Mkondya pekee, inadaiwa kuwa kati ya Januari mosi 2020 na Desemba mosi 2023, jijini Dar es Salaam na akiwa Mkurugenzi wa kampuni hiyo, alijipatia viwanja tisa vilivyopo katika kitalu namba AB, eneo la Idunda, mkoani Njombe. Mkondya anadaiwa kujipatia viwanja hivyo huku akijua ni matokeo ya makosa ya kuendesha biashara ya upatu.
Akiwasomea PH, Wakili Titus amedai kuwa Mkondya ndiye mwenye kampuni hiyo na John akifanya kazi chini ya maelekezo yake. Katika tarehe hizo, Mkondya na John waliendesha biashara ya upatu na kujipatia fedha kutoka kwa watu 117 huku wakiahidi faida mara mbili ya fedha walizotoa.
Fedha hizo zilikuwa zikitumwa kwenye akaunti binafsi ya Mkondya na nyingine katika akaunti ya kampuni iliyopo benki ya CRDB.
Iliendelea kudaiwa kuwa Mkondya baada ya kupata fedha hizo, alinunua viwanja na kuanzisha kilimo cha vanilla Idunda bila kufuata taratibu za Mamlaka za mkoa wa Njombe. Baada ya kilimo hicho kushindwa, Mkondya alihamishia kilimo hicho Zanzibar, lakini hakutimiza ahadi alizotoa kwa walalamikaji.
Hata hivyo, baadaye Mkondya na mwenzake walikamatwa kwa uchunguzi na, ulipokamilika, walipelekwa mahakamani na kushtakiwa kwa kesi ya uhujumu uchumi. Washtakiwa baada ya kusomewa hoja za awali walikubali taarifa zao binafsi, huku wakikana mashtaka yanayowakabili.
“Mheshimiwa Hakimu, upande wa Jamhuri unatarajia kuwa na mashahidi zaidi ya 117 na vielelezo zaidi ya 100, hivyo tunaomba mahakama itupangie kuanza kusikiliza ushahidi,” amedai Wakili Titus.
Hakimu Nyaki amesema kesi hiyo itasikilizwa kwa siku tatu mfululizo kuanzia Januari 20 hadi 23, 2026. Mshtakiwa Mkondya amerudishwa rumande kutokana na kukabiliwa na mashtaka ya kutakatisha fedha.
Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Novemba 5, 2024 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 31523 ya mwaka 2024.
