Morogoro. Miili minne kati ya sita ya ajali ya basi na lori iliyoshindwa kutambulika kwa njia ya kawaida, hatimaye imetambuliwa na ndugu kwa njia ya vinasaba (DNA).
Kwa hatua hiyo, miili miwili imebaki katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro ikisubiri ndugu kwenda kuchukuliwa vinasaba na kuitambua.
Ajali hiyo iliyotokea usiku wa Desemba 31, 2025 eneo la Maseyu barabara ya Morogoro – Dar es Salaam na kusababisha vifo vya watu 10 na majeruhi 23 ambapo miili tisa ilifikishwa hospitalini hapo na mwili mmoja ulihifadhiwa katika kituo cha afya Mikese.
Awali, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema ajali hiyo ilihusisha basi la abiria la Kampuni ya Mawio lililokuwa likitoka Morogoro kwenda Tanga na kugongana na lori la mizigo lililokuwa likitoka Dar es Salaam kuelekea Morogoro kisha kuwaka moto.
Kamanda Mkama katika taarifa yake kwa vyombo vya habari alisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa lori ambaye aliyapita magari ya mbele yake bila ya kuchukua tahadhari.
Akitoa taarifa ya utambuzi wa miili hiyo leo Jumatatu, Januari 5, 2026, Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk Joseph Kway amesema miili mitatu kati ya tisa iliyohifadhiwa hospitalini hapo ilitambuliwa kwa njia ya kawaida, huku miili sita ikishindwa kutambulika kutokana na kuungua kwa kiasi kikubwa.
Amesema iliwalazimu wataalamu kutoka ofisi ya mkemia mkuu wa Serikali kufika hospitalini hapo kwa ajili ya kuchukua sampuli za vinasaba kwenye miili hiyo kwa lengo la kulinganisha na vinasaba vya ndugu watakaoshindwa kutambua marehemu wao.
“Kwa sasa ni miili miwili tu ya ajali hii iliyobaki katika chumba chetu cha kuhifadhi maiti, na mpaka sasa bado hajajitokeza mtu yeyote kutaka kumtambua ndugu yake kwa njia ya DNA, hivyo wataalamu kutoka ofisi ya mkemia mkuu wa Serikali bado wapo wakisubiri ndugu wenye miili iliyobaki,” amesema Dk Kway.
Kuhusu hali za majeruhi, Dk Kway amesema majeruhi waliobaki hospitalini hapo ni wawili ambapo mmoja ameshafanyiwa upasuaji wa kwanza na sasa anasubiri upasuaji wa pili.
“Majeruhi hawa wote hali zao zinaendelea vizuri na bado wataendelea kuwepo hapa hospitali kwa muda mrefu kidogo kwa sababu matibabu yao yanahitaji upasuaji wa awamu,” amesema Dk Kway.
