Miradi 150 ya uwekezaji kusajiliwa Zanzibar kila mwaka

Unguja. Wakati mazingira na miundombinu vikiboreshwa, Zanzibar imepanga kusajili miradi isiyopungua 150 ya uwekezaji kila mwaka kupitia Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA).

Hayo yameelezwa leo, Januari 5, 2026, na Waziri wa Kazi na Uwekezaji, Shariff Ali Shariff, katika siku ya uwekezaji iliyoandaliwa kwenye maonyesho ya Zanzibar International Trade Fair (ZITF) yanayoendelea katika Viwanja vya Maonyesho Nyamanzi, Unguja, Zanzibar.

“Mipango ya Serikali ni kuhakikisha inasajili miradi isiyopungua 150, sawa na miradi 600 kwa miaka mitano ijayo. Kwa hiyo, sisi Serikali tupo tayari na tumeshajipanga kuhakikisha mazingira ya uwekezaji na kibiashara Zanzibar yanaimarishwa,” amesema Shariff.

Amesema katika kipindi kilichopita, wamefanikiwa kusajili miradi 560, ikiyosababisha mtaji wa Dola bilioni 6.8 za Marekani na kutengeneza ajira zaidi ya 28,000.

“Tayari tuna kituo cha One Stop Center pale ZIPA, kinachotoa kila aina ya msaada unaohitajika kwa mwekezaji, ikiwemo usajili wa kampuni, kupata vibali vya ujenzi, hatimiliki za ardhi na vibali vya makazi,” amesema.

Amesema kibali cha kazi kilichokuwa kinachukua siku 30 kwa sasa kinapatikana ndani ya siku moja, wakati mwingine ni saa kadhaa.

Waziri wa Kazi na Uwekezaji Zanzibar, Shariff Ali Shariff akizungunza wakati wa siku ya uwekezaji katika maonyesho ya Zanzibar International Trade Fair (ZITF) katika viwanja vya Nyamanzi, Unguja Zanzibar. Picha na Jesse Mikofu

Kwa mujibu wa Shariff, uchumi wa nchi unategemea zaidi wawekezaji, hivyo watahakikisha wanaisimamia ili wawekezaji wengi zaidi wawekeze.

Amesema sheria ya uwekezaji ya mwaka 2023 ni rafiki, lakini kuna baadhi ya vipengele vinavyohitaji kanuni za utekelezaji, hasa kuhusu ujenzi wa nyumba za biashara na viwanda, ili kuona namna ya kuimarisha viwanda, kuvutia wawekezaji na kusababisha ukuaji wa uchumi na ajira nyingi.

Hata hivyo, amesema bado kuna changamoto ya wawekezaji wa ndani kuona kama uwekezaji ni wa watu kutoka nje ya nchi.

“Tumetekeleza taratibu ili wawekezaji wa ndani wapate vivutio vikubwa zaidi, ambapo kiwango cha chini cha mwekezaji wa ndani ni Dola 50,000 na kutoka nje ni Dola 500,000. Uwekezaji wa ndani unaimarika zaidi. Wananchi waje, fursa zipo,” amesema.

Naye Mkurugenzi wa Zanzibar National Chamber of Commerce (ZNCC), Hamad Hamad, amesema wamepata maarifa kupitia mdahalo huo kwa wafanyabiashara, na kwamba miradi hiyo inaweza kufikiwa kutokana na jinsi Serikali ilivyojipanga kuvutia wawekezaji.

“Muhimu ni kuzingatia namna ya kuhifadhi mazingira na tamaduni zetu, maana kadri wanavyokuja ni rahisi kupoteza urithi na uendelevu,” amesema Hamad.

Amesema mkazo mkubwa umewekwa kwa wawekezaji wa nje, lakini wanapaswa kutoa kipaumbele kwa wazawa, kwani biashara inapoendeshwa na wenyeji inazalisha ajira za kudumu. Pia, inapaswa kuwahamasisha na kuwapa motisha kuwekeza zaidi.

Washiriki wa Mdahalo wa siku ya Uwekezaji katika maonyesho ya Zanzibar International Trade Fair katika viwanja vya maonyesho Nyamanzi, Unguja Zanzibar. Picha na Jesse Mikofu

Kadhalika, amesema kuna haja ya kutoa ushirikiano kati ya taasisi za Serikali na sekta binafsi, akitaja maeneo kadhaa ikiwemo mawasiliano kati ya sekta binafsi na Serikali.

“Mfano, kuna mabadiliko ya sheria na kanuni yanatokea, lakini hakuna mawasiliano ya moja kwa moja kutoka serikalini kueleza sekta binafsi kuwa jambo limefanyika. Baada ya muda, unamsikia mwekezaji akisema hali imebadilika, hivyo si mazingira mazuri kwa mwekezaji kwani hayatabiriki,” amesema.

Naye Kamishna wa Idara ya Walipakodi Wakubwa kutoka Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA), Shaaban Jafar Jumanne, amesema kuna punguzo la kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kutoka asilimia 18 hadi 15, lengo likiwa kuvutia wawekezaji.

Amesema ili kuwavutia wawekezaji, wamejenga mifumo imara zaidi ya ukusanyaji wa kodi, kwani wanatoka katika nchi zenye maendeleo tofauti na wanapendelea kutumia mfumo wa ulipaji wa kodi unaofaa, rahisi na unaoondoa usumbufu.

“Kwa hiyo, tumejipanga zaidi kutumia mifumo ya ulipaji wa kodi ili kuwawekea unafuu, na kutopoteza muda. Kwa sasa anajisajili mtandaoni, anafanya kila kitu akiwa sehemu yake ya biashara,” amesema.

Shaaban amesema wanategemea, ikiwezekana, hata malalamiko yote yanayohusiana na ZRA yawe yanapewa huduma mtandaoni ili kumpa muda mwekezaji kufanya shughuli za kiuchumi badala ya kupoteza muda ofisini.

Naye Mkurugenzi wa Mipango ya Uwekezaji, Al Haji Jecha, ameishauri ZRA kuweka ofisi ZIPA ili kuwapa unafuu wanaokwenda kusajili miradi na kupata huduma zote pale pale.