Mpanzu, Sowah freshi Simba, Ahoua Mmh!

KULE Simba winga Ellie Mpanzu amejisalimisha fasta ndani ya muda ambao ulitolewa lakini Jonathan Sowah akichelewa kwa siku moja huku Jean Charles Ahoua akizua utata.

Kocha Barker alitoa siku tatu kwa wachezaji wake ambao walikuwa kwenye mapumziko nje ya wale waliokuwa kwenye ushiriki wa Fainali za Mataifa Afrika kuwahi kambini.

Kuanzia tangazo hilo lilipotoka Mpanzu fasta akajisalimisha akirejea kwenye timu hiyo juzi na jana akaanza kujifua chini ya Barker huku Sowah akitua jana alfajiri.

Hata hivyo, Ahoua alikuwa awasili juzi Januari 3, lakini mpaka jana mchana bado alikuwa hajawasili nchini.

Bosi mmoja wa Simba ameliambia Mwanaspoti kuwa kiungo huyo ana saa 24 tu za kurekebisha uchelewaji wake ambapo endapo atashindwa kuwasili jana Januari 4, basi anaweza kukumbana na adhabu.

SIMBA 01

“Ahoua ndio bado hajafika na alitakiwa afike hapa Januari 3, sijajua kipi kinaendelea,” amesema bosi huyo.

“Sowah alifika alfajiri ya jana lakini bado hajakwenda Zanzibar kuungana na wenzake ingawa amechelewa kutokana na muda aliotakiwa kufika, tutajua baadaye kama kuna hatua zitachukuliwa.

“Unaweza kumwelewa kama atafika Januari 4 lakini kama atachelewa zaidi ya hapo haitakuwa rahisi kupokewa vizuri, hii ni timu na moja ya vitu ambavyo huyu kocha (Barker) anataka kuvifanyia kazi ni nidhamu ya timu nzima.

“Ukiacha hilo unajua kwamba muda huu hizi mechi za Mapinduzi, kocha anataka kumfahamu kila mchezaji wake sasa wanapochelewa tunampa shida ya kufanya mambo yake kwa wakati.

Barker amezuia usajili ndani ya kikosi chake akitaka kwanza kutangulia kujua ubora halisi wa wachezaji wake kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho.

Simba itarudi uwanjani leo kucheza mchezo wake wa pili kwenye Kombe la Mapinduzi dhidi ya Fufuni SC, baada ya kushinda mechi ya kwanza 1-0.

SIMBA 02

BARKER APEWA MASHINE TATU

Katika hatua nyingine juzi Simba ilipokuwa ikiichapa Muembe Makumbi City kwa bao 1-0 katika mechi ya kwanza ya Kombe la Mapinduzi kwa Wekundu hao waliopo Kundi B kuna nyota watatu waliibuka kikosini na inaelezwa kocha Steve Barker ameletewa ili awasome kabla ya kuwapa mikataba kuitumikia timu hiyo.

Katika mechi hiyo, Simba ilimuanzisha straika Baraka Mwangosi aliyetokea Mbeya City, huku benchi akiwapo Bright Anukani kutoka KCCA ya Uganda na Charles Ouma Sila wa Kenya Police ikielezwa wapo katika majaribio ili kama watamridhisha Barker na benchi lake watasajiliwa rasmi kupitia dirisha dogo litakalofungwa Januari 30.

Mmoja wa maofisa wa Simba, aliliambia Mwanaspoti, Mwangosi yupo kwenye mazungumzo mazuri ya kupewa mkataba na hata nafasi aliyopewa kucheza kwa dakika zote 90, ulikuwa mpango wa kocha Barker kujiridhisha zaidi uwezo wake.

SIMB 03

“Umemuona Mwangosi, hana hata muda mrefu wa kufanya mazoezi na timu lakini mchezaji mzuri anaonekana tu. Anajua kukaa kwenye maeneo kama mshambuliaji, hivyo kuna asilimia kubwa ya kupewa mkataba kwani hivi sasa bado hajasajiliwa,” amesema bosi huyo.

Kwa upande wa Anukani anayecheza nafasi ya kiungo mshambuliaji, juzi hakupata nafasi, hivyo kuna uwezekano leo Jumatatu dhidi ya Fufuni, akakiwasha.

Kiungo huyo raia wa Uganda mwenye umri wa miaka 25 naye anaangaliwa kabla ya kupewa mkataba wa kuitumikia Simba, ilihali Sila ni raia wa Sudan Kusini mwenye umri wa miaka 26 akicheza nafasi ya kiungo mkabaji eneo lina Mzamiru Yassin, Yusuph Kagoma na Naby Camara ambaye wakati mwingine huchezeshwa beki wa kushoto.