Mradi wa EACOP wafikia asilimia 79, kukamilika Julai 2026

Dar es Salaam. Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi amesema mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga (EACOP) umefikia asilimia 79 na utakamilika Julai 2026.

Kukamilika kwa mradi huo ni baada ya takribani miaka 10 ya utekelezaji wake unaohusisha ujenzi wa bomba la inchi 24 lenye urefu wa kilomita 1,443 lenye uwezo wa kusafirisha mapipa 216,000 ya mafuta ghafi.

Mradi huo upo chini ya wanahisa Kampuni ya Total Energy yenye hisa asilimia 62, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanznaia (TPDC) asilimia 15, UNOC asilimia 15 na CNOOC asilimia 8.

Waziri wa Nishati wa Tanzania, Deogratius Ndejembi akizungumza leo Jumatatu, Januari 5, 2026 jijini Dar es Salaam, katika mkutano na waandishi wa habari.

Akizungumza leo Jumatatu, Januari 5, 2026 jijini Dar es Salaam, katika mkutano na waandishi wa habari, kufuatia ziara ya viongozi mbalimbali wa Uganda kutembelea mradi wa ECOP, Ndejembi amesema mradi huo ni muhimu kwa Tanzania na Uganda.

“Kwa miaka 10 sasa mradi huu tangu uanze mwaka 2016 sasa utakwenda kukamilika Julai 2026, hadi sasa tumefikia asilimia 79 na bado asilimia 21 ambayo tutaikamilisha Julai mwaka huu na suala la kuanza kwa mradi hii itakuwa,” amesema.

Amesema Serikali ya Tanzania imewekeza fedha nyingi kwenye mradi huo kuhakikisha unakamilika kwa wakati.

Akizungumzia manufaa ya mradi wa EACOP, Ndejembi amesema kupitia mradi huo zaidi ya ajira 10,000 zimetengenezwa, wataalamu wa ndani kupatiwa ujuzi ambao wanakwenda kutumia maeneo mengine.

“Kuna vituo vinne vitakuwa hapa nchini na uchumi wa maeneo hayo utaimarika na Mkoa wa Tanga ambao mradi umepita utaendelea kukua kiuchumi,” amesema.

Waziri wa Nishati na Mandeleo ya Madini wa Uganda, Dk Ruth Nankabirwa amesema ziara ya viongozi wa mradi wa Bomba la EACOP imelenga kujionea utekelezaji halisi wa mradi badala ya kutegemea taarifa za karatasi pekee.

Akieleza kuhusu maandalizi ya miundombinu, amesema mabomba ya mafuta yamewekewa kinga maalumu katika Mkoa wa Tabora kutokana na asili ya mafuta ya Uganda kuwa na nta.

 “Kwa kuwa mafuta yetu yana nta lazima yapashwe joto, ndiyo maana tulilazimika kuyawekea ‘insulation’ ili kulinda mazingira,” amesema.

Kuhusu uzalishaji wa mafuta, amesema shughuli za utafutaji na uchimbaji zinaendelea vizuri upande wa juu wa mradi, zikiongozwa na kampuni za TotalEnergies na CNOOC.

“Wamechimba visima vingi vyenye uzalishaji mzuri kuliko hata tulivyotarajia, mapipa 60,000 kwa siku yatasafishwa ndani ya nchi huku mapipa 190,000 yakipelekwa kwenye masoko ya kimataifa,”amesema.

Waziri huyo amesisitiza umuhimu wa maandalizi ya hifadhi ya mafuta ghafi ili kuepusha changamoto za kibiashara.

“Hatutaki kuzalisha mafuta bila kuwa na mahali pa kuyahifadhi, ndiyo maana hifadhi ya mafuta itakuwa Tanga kwa ajili ya usafirishaji wa kibiashara,” amesema.

Waziri Nankabirwa amesema Serikali ya Tanzania imekuwa mshirika wa kuaminika na wa kimkakati ardhi na mahitaji yote muhimu yalipatikana kwa wakati,akisisitiza kuwa mradi wa EACOP umevutia uwekezaji wa takribani Dola 4 bilioni za Marekani.