Naibu Waziri awataka vijana kutokubadilishwa na desturi za kigeni

Arusha. Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir, amewataka vijana 50 waliofaulu kwa ngazi ya juu na kupata ufadhili kupitia mpango wa Samia Scholarship Extended nje ya nchi, kuwa wazalendo na kurejea kuwatumia Watanzania.

Amesema hayo leo Jumatatu, Januari 5, 2025, katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST), kuwa kuwapata vijana hao ni matokeo ya mchujo mkali uliotokana na sifa za ufaulu wao.

Wanu, ambaye ni mara yake ya kwanza kufika katika taasisi hiyo inayotoa shahada za umahiri na uzamili pekee katika sayansi na ubunifu, amesema Serikali imedhamiria kuwapa ujuzi vijana ili wawe na uwezo katika ushindani wa ajira za ndani na nje ya nchi.

“Nimefurahi sana kuwaona vijana ambao mmechaguliwa kusoma nje ya nchi kwenye kada ambazo Serikali imezipa kipaumbele, ili mtakaporejea muwe chachu ya kutatua changamoto zilizopo, mkiwa masomo zingatieni maadili ya Kitanzania na kukumbuka ‘msahau kwao ni mtumwa’,” amesema Wanu.

Katika ziara yake hiyo, pia, amekagua ujenzi wa jengo la hosteli ulioanza mwaka 2021, linalojengwa kwa awamu tatu, huku awamu ya kwanza ikitarajiwa kukamilika Aprili 2026 kwa fedha za Serikali Kuu, Sh6.2 bilioni.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir (kushoto) akiongozana na Makamu Mkuu wa taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST), Profesa Maulilio Kipanyula akikagua ujenzi wa hosteli za wanafunzi. Picha na Filbert Rweyemamu

Pia, ameutaka uongozi wa taasisi hiyo kuwasaidia vijana watakaochaguliwa msimu ujao kuwatafutia ufadhili wa masomo nje ya nchi, ili kuipa Serikali nafasi ya kuwahudumia wananchi wengine.

Naibu Waziri huyo ameagiza ujenzi ukamilike kwa wakati, kuzingatia viwango vya ubora na kuakisi hadhi ya taasisi hiyo, ili itoe nafasi kupokea wadahiliwa wengi zaidi.

“Kama mlivyonieleza, pamoja na sababu nyingine, ni kuongeza udahili kwa wanafunzi wa kike ambao wako kwenye majukumu ya familia, wanaweza kuendelea na masomo wakiwa na watoto wao hapa chuoni. Mpango wa Serikali unaoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ni kutokumwacha mtu yeyote nyuma,” amesema Wanu.

Awali, makamu mkuu wa taasisi hiyo, Profesa Maulilio Kipanyula, amesema mpango wa Samia Scholarship Extended, unaosimamiwa kwa ushirikiano na Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), unawapa mafunzo ya wiki 10 kwenye kambi maalumu iliyopo kwenye taasisi hiyo.

Amesema vijana hao wamepata ufadhili kwenye kozi za Sayansi ya Takwimu, Akili Unde na Sayansi Shirikishi, kwenye Chuo Kikuu cha Johannesburg, Afrika Kusini, na Limerick, nchini Ireland.

“Vijana hawa wanaendelea kupata mafunzo mbalimbali kwenye kambi hii, ikiwemo namna ya kuomba ufadhili wa masomo nje ya nchi, mila na tamaduni za nchi wanazoenda kusoma, pia uzalendo na usalama yaliyotolewa na viongozi wabobezi,” amesema Profesa Kipanyula.

Kuhusu ujenzi wa hosteli, amesema awamu ya kwanza imefikia asilimia 80, na lengo ni kwamba, utakapokamilika awamu zote tatu, taasisi hiyo itaweza kudahili wanafunzi 1,000 kutoka kiwango cha sasa cha wanafunzi 600.