Samia: Tuzo za utalii ni matokeo ya uhifadhi, mshikamano

Zanzibar. Rais Samia Suluhu Hassan, amesema mafanikio ya Tanzania kuendelea kutwaa tuzo za kimataifa za utalii yanatokana na uwekezaji wa muda katika uhifadhi wa rasilimali asilia, mshikamano wa wadau na juhudi za makusudi za kuitangaza nchi kimataifa.

Hayo amesema leo, Jumatatu Januari 5, 2026 baada ya kupokea tuzo tatu za kimataifa za utalii, Ikulu ya Tunguu, Zanzibar.

Amesema ushindi huo si wa bahati, bali ni matokeo ya kazi endelevu inayofanywa na taasisi za Serikali, sekta binafsi na jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi.

Ameeleza vivutio vya utalii nchini vinaendelea kuvutia wageni kutokana na mchanganyiko wa rasilimali za kipekee wakiwamo wanyamapori, mandhari ya asili, maji, amani na ukarimu wa Watanzania, akisisitiza sifa hizo ndizo zinazoipa Tanzania nafasi ya ushindani duniani.

Rais Samia amewapongeza wataalamu wa uhifadhi na utalii kwa kulinda vivutio hivyo na kusimamia kwa weledi rasilimali zilizopo.

Amesema Serikali itaendelea kuimarisha sera na miundombinu itakayoongeza thamani ya sekta ya utalii na mchango wake katika uchumi wa Taifa.

Ameongeza tuzo hizo ni uthibitisho wa kuimarika kwa taswira ya Tanzania kimataifa na ishara ya kuongezeka kwa imani ya wawekezaji na watalii, hali inayochochea ukuaji wa uchumi, ajira na mapato ya fedha za kigeni.

Katika hafla hiyo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji, alimkabidhi Rais tuzo hizo tatu kwa niaba ya Serikali na wadau wa utalii, akieleza kuwa Tanzania ilitunukiwa tuzo mbalimbali.

Tuzo ambazo Tanzania ilitunukiwa ni Kituo Bora cha Utalii wa Safari Duniani na Hifadhi Bora Duniani, huku nchi pia ikitajwa kuwa Kituo Bora cha Utalii Barani Afrika mwaka 2025.

Kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), sekta ya utalii iliendelea kuimarika mwaka 2025. Idadi ya watalii iliongezeka kwa zaidi ya asilimia tisa na mapato kufikia Dola 4.2 bilioni za Marekani ikiwa ni ishara ya mchango mkubwa wa sekta hiyo katika maendeleo ya Taifa.