MSHAMBULIAJI wa Zimamoto ya Zanzibar, Seleman Mgaza ameziingiza vitani timu mbili za maafande wa JKT Tanzania na KMC, ambazo zimeonyesha nia ya kumhitaji katika dirisha hili dogo, huku mazungumzo kati ya pande hizo yakiendelea.
Taarifa ambazo Mwanaspoti limezipata zinaeleza Mgaza ambaye katika dirisha lililopita alikuwa akihitajika na Geita Gold na TRA United (zamani Tabora United), ameonyesha utayari wa kucheza Ligi Kuu Bara na kinachosubiriwa ni makubaliano.
Hata hivyo, Mwanaspoti linatambua JKT ndio timu ya kwanza kuwasiliana na wawakilishi wa mchezaji huyo, ingawa itakutana na ushindani mkubwa kutoka kwa KMC kutokana na uhusiano wa Mgaza na Kocha Abdallah Mohamed ‘Baresi’ aliyemfundisha.
Baresi aliyejiunga na KMC Desemba 30, 2025 akichukua nafasi ya Mbrazili Marcio Maximo, alifanya kazi na nyota huyo wakiwa Zimamoto kabla ya kujiunga na kikosi hicho cha Kinondoni, jambo linaloweza kurahisisha dili hilo ili waungane tena.
Mwanaspoti linatambua kwamba katika mapendekezo ya Baresi kwenye kikosi hicho ni kuongezewa mshambuliaji mwingine wa kuongeza nguvu kwani hadi sasa KMC iliyopo mkiani safu ya ushambuliaji imefunga mabao mawili tu katika mechi tisa za Ligi Kuu.
Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa KMC, Daniel Madenyeka amesema bado wanaendelea kupitia ripoti ya benchi la ufundi ili kuboresha maeneo mbalimbali ya kikosi hicho, japo ni mapema kwa sasa kuzungumzia ni mchezaji gani watakayemsajili.
