WAKIJIANDAA kwa mechi ya mwisho kuhitimisha kundi A ambayo imebeba hatma ya kila mmoja wao, nyota wa URA, Mulikyi Hudu ameitumia salamu Azam FC kwa kusema, ijiandae kupokea maumivu na si kingine.
Timu hizo zitakutana leo Jumatatu saa 10:15 jioni kwenye Uwanja wa New Amaan Unguja katika Kombe la Mapinduzi.
Hudu ambaye alitangazwa kuwa mchezaji aliyeonyesha mchezo wa kiungwana katika mechi dhidi ya Singida Black Stars, amesema tuzo hiyo imempa nguvu zaidi ya kwenda kupambana dhidi ya Azam.
Amesema wanahitaji zaidi ushindi katika mechi ijayo hivyo hawana budi kujiandaa vizuri na wapinzani wao watarajie maumivu.
“Nashukuru kwa tuzo hii ambayo imenipa nguvu zaidi ya kufanya mechi ijayo na kuhakikisha tunashinda dhidi ya Azam.
“Michuano hii tunataka kufanya vizuri, hivyo ili tuendelee lazima tuifunge Azam na tunakwenda kujiandaa kwa hilo. Tunataka kushinda,” amesema Hudu.
Katika msimamo wa kundi A, URA na Azam kila moja ina pointi nne, Singida (5).
Singida BS imetangulia nusu fainali ikiacha msala kwa wawili hao.
URA inahitaji ushindi pekee ili kufuzu nusu fainali, wakati Azam hata sare inawabeba kwani hivi sasa ipo juu ya mpinzani wake kwa tofauti ya bao moja. Azam imefunga matatu na kuruhusu moja, URA inayo mawili na imeruhusu moja.
