Starlink yasitisha huduma za intaneti Uganda

Kampala. Mtoa huduma wa intaneti ya setilaiti, Starlink, amesitisha upatikanaji wa mtandao wake wa kimataifa nchini Uganda.

Hatua hiyo imesababisha vifaa vyote vya Starlink vilivyokuwa vinatumika nchini humo kusitisha kazi kuanzia Januari 1, 2026, kufuatia agizo la Tume ya Mawasiliano ya Uganda (UCC) kuhusu matumizi ya huduma za setilaiti zisizo na leseni.

Katika barua ya Januari 2, mwaka huu, Starlink ilithibitisha iliwasilisha na kuanzisha mfumo wa kuzuia huduma ili kuzuia kabisa upatikanaji wa intaneti ya setilaiti ndani ya Uganda.

Barua hiyo, iliyosainiwa na Ben MacWilliams, Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Teknolojia ya Utafiti wa Anga, ilielekezwa kwa Mkurugenzi Mtendaji wa UCC, ikiwa ni majibu ya hoja zilizotolewa kuhusu matumizi haramu ya huduma za intaneti ya setilaiti nchini humo.

Starlink inaeleza kuwa haiuzi, haitangazi wala haitoi moja kwa moja huduma za intaneti ya setilaiti nchini Uganda, na kwamba hakuna vifaa vya Starlink vilivyoingizwa au kusambazwa rasmi nchini humo.

“Ili kuweka wazi, Starlink Uganda yenyewe haiuzi wala haitangazi huduma za intaneti ya setilaiti nchini Uganda kwa kuwa bado haijapatiwa leseni na UCC,” inaeleza kampuni hiyo.

Kwa mujibu wa Starlink, upatikanaji wa huduma hiyo nchini Uganda kabla ya kusitishwa uliwezeshwa kupitia vifaa vilivyonunuliwa na kuanzishwa matumizi katika nchi ambazo Starlink imeidhinishwa kisheria, kisha baadaye kuingizwa Uganda bila ruhusa.

Kampuni inasisitiza matumizi hayo yalikiuka masharti yake ya huduma na yalifanyika bila kushirikishwa au idhini yake.

“Huduma za Starlink nchini Uganda zilikuwa zikitumika bila idhini au ridhaa yetu na kinyume cha masharti yetu ya huduma,” inabainisha barua hiyo.

Starlink pia ilithibitisha kufuatia utekelezaji wa hatua hiyo Januari  mosi, mwaka huu, kwa sasa hakuna kifaa chochote cha Starlink kinachoendelea kufanya kazi nchini Uganda.

“Kutokana na hatua zilizochukuliwa kuanzia Januari mosi, hakuna tena vifaa vya Starlink vinavyofanya kazi nchini Uganda,” inaeleza kampuni hiyo, ikisisitiza tena kuwa haijawahi kuingiza wala kusambaza vifaa hivyo nchini humo.

Kusitishwa kwa huduma hiyo kumekuja kufuatia agizo la Desemba 19, 2025, kutoka Mamlaka ya Mapato ya Uganda, lililozuia uingizaji na utoaji wa vibali vya forodha kwa vifaa vya Starlink na mitambo mingine inayohusiana na mawasiliano.

Chini ya agizo hilo, kifaa chochote cha Starlink kinachoingia nchini humo sasa kinapaswa kupata kibali kutoka kwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, hatua inayoweka teknolojia hiyo chini ya usimamizi wa kijeshi.

Muda wa kusitishwa kwa huduma hiyo, ukiwa ni wiki chache tu kabla ya uchaguzi wa Uganda uliopangwa kufanyika Januari 15, mwaka huu, umeibua mjadala mpana kuhusu udhibiti wa huduma za intaneti ya setilaiti, ambazo hufanya kazi bila kutegemea miundombinu ya kitaifa ya nyaya za mawasiliano au mitandao ya simu.

Wachambuzi wanaeleza huduma kama hizi zina uwezo wa kuathiri upatikanaji wa taarifa katika nyakati nyeti za kisiasa.

Pamoja na vikwazo vya sasa, Starlink imeonesha utayari wake wa kushirikiana na wadhibiti wa mawasiliano ili kuwezesha uendeshaji halali wa huduma zake siku zijazo.

“Starlink imejizatiti kushirikiana na mahitaji ya kisheria ya UCC tunapoendelea kukamilisha mchakato wa kupata leseni nchini Uganda,” inaeleza kampuni hiyo.