SAFARI ya wanariadha wa kikosi cha timu ya taifa ya riadha ya Tanzania kushiriki mbio za dunia za Nyika imeiva baada ya kuagwa leo Januari 5, 2026 huku ikitabiriwa kurudi na medali ya dhahabu.
Mashindano hayo yatafanyika Januari 10, 2026, Florida nchini Marekani, ambapo Tanzania itawakilishwa na wanariadha tisa ambao wanatarajiwa kuondoka kesho Jumanne wakiongozwa na bingwa wa marathoni wa taifa, Gabriel Geay kama nahodha wa timu.
Timu hiyo itashiriki katika makundi mawili ambayo ni senior men (kilomita 10), na relay mchanganyiko yenye wanaume wawili sawa na wanawake.
Katika mbio za kilomita 10 kwa wanaume, Tanzania itawakilishwa na Gabriel Geay, Emanuel Dinday, Benjamin Fernandi, Inyasi Sule na John Wele, upande wa relay mchanganyiko, timu itakuwa na Daniel Sinda, Ambrose Ama, Regina Mpiga Chai na Elizabeth Ilanda.
Timu hiyo pia itamkosa kocha wake Andrew Panga na viongozi wengine ambao nao walitarajiwa kusafiri baada ya kukosa pasi ya kusafiria (VISA) ya kuingia nchini Marekani, hivyo kuilazimu Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) kumtumia meneja wa mwanariadha Alphonce Simbu, Derick Froud kuokoa jahazi kama kocha mkuu na tayari amepata uthibitisho kutoka Shirikisho la Riadha la Dunia.
Akikabidhi bendera ya taifa kwa timu hiyo katika halfa fupi ya kuiaga ambayo imefanyika jijini Arusha, Afisa Michezo wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Charles Maguzu, amesema kuna matumaini kibao kuwa watakwenda kurudi na medali kutokana na namna ambavyo wamefanya maandalizi.
“Bendera ambayo tutawakabidhi sisi ni alama ya ushindi na uzalendo wa hali ya juu, ukikabidhiwa bendera ya nchi hakikisha unakwenda kupambana kufa au kupona ili uweze kuilinda heshima ya bendera hiyo,” amesema Maguzu.
Ametumia fursa hiyo kuwaomba wadau mbalimbali wenye nia ya kusapoti wanariadha hao kufika katika ofisi za BMT au RT, kutoa motisha ambayo itawafanya nyota hao ambao wanakwenda kuwakilisha zaidi ya watu milioni 60 kupambana zaidi na kurudi na medali.
Bingwa wa marathoni wa dunia na mwanariadha wa kwanza kushinda medali ya dhahabu ya mashindano ya dunia kwa Tanzania, Alphonce Simbu amewaasa nyota hao kutanguliza uzalendo mbele na kuweka wazi kuwa kutokana na ubora ulioonyeshwa na timu hiyo katika mashindano ya taifa yaliyofanyika Madunga wilayani Babati katika Mkoa wa Manyara, basi watakwenda kurudi na medali ya kwanza ya dhahabu ya mbio za Nyika na kuweka rekodi mpya kwa Tanzania.
Kwa upande wake nahodha wa timu hiyo, Gabriel Geay amesema wamefanya maandalizi ya kutosha na wachezaji wenzake nao wako katika ari kubwa, kilichobaki ni kwenda kufanyia kazi kile ambacho wametumwa kwenda nchini Marekani kukifanya kwa maana ya kurudi na medali.
“Nina uzoefu kwenye mbio hizi za dunia za nyika na nimeshiriki mara kadhaa, kwa mara nyingine tena naenda kuiwakilisha taifa kwa hiari yangu mwenyewe bila kushinikizwa na mtu yeyote, naamini tutaenda kufanya jambo kubwa litakaloiweka nchi kwenye ramani nzuri”, amesema Geay.
Rais wa RT, Rogath John Stephen Akhwari amefunguka kuwa maandalizi yalifanyika vyema kwa kuzingatia mazingira ya sehemu ambayo wanakwenda kushindana ambapo licha ya kuwa ushindani utakuwepo lakini wanariadha wa Tanzania wameandaliwa kwa ajili ya kwenda kushinda, akiamini kama ilivyokuwa mwaka 2025, mafanikio hayo yatahamia pia 2026.
Ameongeza wanariadha hao tisa wanatokea katika taasisi na klabu mbalimbali, ambapo Geay, Dinday, Wele na Fernandi wanatokea Gabriel Geay Athletics, Daniel SindaSinda kutoka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Ambrose Ama kutoka Polisi Tanzania, Inyasi Sule kutoka JWTZ, huku Regina Mpiga Chai na Elizabeth Ilanda ambao wanasoma katika vyuo vikuu nchini Marekani.
Tanzania inaingia katika mashindano haya ikiwa na historia nzuri ya mafanikio, ikiwemo medali ya dhahabu aliyopata Andrew Sambu mwaka 1991 kwa upande wa junior, nafasi ya nne ya Andrew Panga, medali ya fedha ya John Yuda mwaka 2022 nchini Ireland, pamoja na kushika nafasi ya tatu na ya nne.
Mara ya mwisho kushiriki mwaka 2023, Tanzania ilimaliza katika nafasi ya nane kwa ujumla kama timu na sasa ikitaka kutwaa medali ya dhahabu ambayo haijawahi kupata.
