JIONI ya jana Yanga ilishuka uwanjani kutupa karata ya kwanza katika michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex ikivaana KVZ, lakini mapema mastaa wapya watatu waliotua katika dirisha dogo la usajili wameanza na moto na kuleta tumaini jipya kambini mwa timu hiyo.
Yanga imeshawatambulisha wachezaji wawili kati ya watatu wapya waliopo na kikosi hicho katika michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026 akiwamo Emmanuel Mwanengo aliyetokea TRA United, Marouf Tchakei na Mohamed Damaro wote wakitokea Singida Black Stars.
Mwanengo alikuwa wa kwanza kutambulishwa na Yanga akipewa mkataba wa hadi 2028 kisha kufuatiwa na Damaro ambaye ametua kwa mkopo hadi mwisho wa msimu huu, huku Tchakei hadi jana mchana alikuwa hajatambulishwa rasmi, lakini naye amechukuliwa kwa mkopo.
Juzi Jumamosi mara baada ya kutua visiwani hapa, nyota hao watatu pamoja na wachezaji wengine wa Yanga walifanya mazoezi, huku Tchakei na Damaro wakimpa jeuri kocha Pedro Goncalves kwa jinsi walivyoongeza nguvu kikosini.
Mwanaspoti lilikuwapo katika mazoezi ya kujiandaa na mechi hiyo ya jana kwa muda wa dakika 15 na kushuhudiwa wachezaji hao wakifanya yao na baada ya kutolewa, bado lilifuatilia kupitia vyanzo vyake kwenye Uwanja wa Amaan na kudokezwa watatu hao walionyesha wametua na kitu kipya kikosini na kumkuna Pedro.
Baada ya mazoezi hayo, chanzo kimeliambia Mwanaspoti, viungo hao wanaocheza nafasi ya ukabaji (Damaro) na ushambuliaji (Mwanengo na Tchakei) wamempa jeuri kocha kwa namna walivyokuwa wakitekeleza kwa ufanisi maelekeo sambamba na wenzao pamoja na kuonyesha vitu adimu mazoezini hapo.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, namna ambavyo wachezaji hao wamefika na kufanya mazoezi kwa nguvu, imetoa imani kwamba kikosi kinazidi kuwa imara kuelekea mechi zijazo za mashindano yote kwa kuanza na Mapinduzi, Ligi ya Mabingwa Afrika na Ligi Kuu hapo baadaye itakapoendelea.
“Tulikuwa nao mazoezini tangu Dar, kwa siku ambazo kocha amewaona mazoezini ameonyesha kuridhika na usajili wao, kwani watasaidia katika kufikia malengo ya timu.
“Eneo la kiungo cha chini kulikuwa na changamoto tangu kuondoka kwa Aucho (Khalid) na hata aliyesajiliwa ameonekana bado anahitaji muda kuzoea, lakini kwa siku chache alizokuja Damaro, ameonyesha tofauti, tusubiri tumuone katika mechi za mashindano,” kilisema chanzo chetu cha habari na kuongeza;
“Tchakei anasaidia eneo la ushambuliaji sambamba na Mwanengo ambao wote hao hakuna asiyewafahamu walivyokuwa wakifanya walipotoka. Niseme tu, tumepata watu wa maana.”
Usajili wa Damaro aliyeingia kama mchezaji mzawa baada ya Januari 2025 kubadili uraia kutoka Guinea hadi Tanzania, unatajwa kuja kusaidia eneo hilo la kiungo cha ukabaji baada ya Aziz Andabwile na Moussa Balla Conte kushindwa kuleta maajabu na kumfanya Pedro kuwatumia Duke Abuya.
Tchakei, raia wa Togo, anaingia kama mchezaji wa kigeni akichukua nafasi ya Andy Boyeli, huku Mohamed Doumbia ambaye hajaonekana na kikosi hicho cha Yanga kilichotua Zanzibar ikielezwa anatolewa dirisha hili dogo, nafasi yake ataingizwa Yao Kouassi, beki wa kulia aliyechomolewa katika usajili wa dirisha kubwa ili kumpa muda zaidi wa kupona na sasa yupo fiti kuendelea kuutumikia mkataba wake utakaoisha mwisho wa msimu huu.
Yanga inaitumia michuano ya Kombe la Mapinduzi ambapo kesho itamalizana na TRA United ili kujiandaa na mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika zitakazopigwa mwishoni mwa mwezi huu dhidi ya Al Ahly ya Misri inaoongoza msimamo wa Kundi B kwa tofauti na mabao ya kufunga na kufungwa licha ya kulingana pointi nne na Yanga.
MZIZE AONGEZA MZUKA YANGA
Mshambuliaji kinara wa mabao ndani ya Yanga kwa msimu uliopita, Clement Mzize ameongeza mzuka ndani ya kikosi hicho kufuatia kuonekana mazoezini akirejea kwa kasi.
Mzize aliyeumia goti tangu Septemba mwaka jana katika mechi ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wiliete Banguela ya Angola ambapo Yanga ilishinda kwa mabao 3-0 kisha kufanyiwa upasuaji Novemba hivi sasa yupo na kikosi cha timu hiyo hapa Unguja kwa ajili ya mashindano ya Kombe la Mapinduzi 2026.
Mshambuliaji huyo aliyemaliza na mabao 14 katika Ligi Kuu Bara msimu uliopita, nyuma ya kinara Jean Charles Ahoua wa Simba aliyekuwa nayo 16, kurejea kwake mazoezini kwa kasi kumeibua tumaini jipya kuelekea mechi nne za michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika zilizobaki hatua ya makundi dhidi ya Al Ahly ugenini na nyumbani, AS FAR Rabat (ugenini) na JS Kabylie (nyumbani).
Chanzo kutoka katika kambi ya Yanga hapa Unguja, kimesema kwa sasa Mzize amepewa programu maalum ya mazoezi ya kukimbia na kuchezea mpira kabla ya kuungana na wenzake rasmi.
Mtoa taarifa huyo amesema, kuna uwezekano mkubwa Mzize akawahi moja kati ya mechi mbili zijazo za CAF dhidi ya Al Ahly kutokana na kasi ya uponaji wake tofauti na hofu iliyokuwapo mwanzoni kwamba huenda akaonekana uwanjani Februari na kuwa katika hatihati ya kuzicheza mechi zote za makundi zilizosalia kwa Yanga.
“Alianza mazoezi taratibu tangu Desemba mwaka jana ndio maana tumekuja naye huku Zanzibar ili aendelee na programu za mazoezi za uwanjani baada ya awali kuanzia gym. Anaendelea vizuri na amekuwa akikimbia na kuchezea mpira, matarajio yetu katika wiki mbili hadi tatu zijazo ataungana rasmi na wenzake kufanya mazoezi ya jumla,” kimesema chanzo hicho.
Januari 23, 2026, Yanga itakuwa nchini Misri kucheza dhidi ya Al Ahly, kisha zitarudiana Januari 30, 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja zikiwa ni mechi za kundi B katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Baada ya hapo, Februari 6, 2026, itacheza na AS FAR Rabat nchini Morocco na Februari 14, 2026 itaikaribisha JS Kabylie.
Hatua ya Mzize kurejea kwa kasi, imeelezwa umeufanya hata uongozi wa Yanga kufikiria kusitisha mpango wa kusajili mshambuliaji mwingine baada ya kuona maendeleo mazuri ya Mzize, huku kocha Pedro Gonclaves akimsubiri kwa hamu kuanza kumtumia nyota huyo kwani hajamfaidi tangu atue.
