Tofauti ya mishahara kwa madaktari yamuibua Waziri Mchengerwa, atoa maelekezo

Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa amewaelekeza Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kuanza mapitio ya mishahara na maslahi ya watumishi wa sekta ya afya, akisema haiwezekani kuwepo kwa tofauti kubwa ya mishahara baina ya watumishi wenye elimu inayofanana.

Mchengerwa amesema ni jambo lisilowezekana daktari bingwa anayefanya kazi sekta ya afya Tamisemi apitwe mshahara kwa kiwango kikubwa na daktari wa ngazi ya kati anayefanya kazi ndani ya Wizara ya Afya.

Amesema mapitio hayo yalenge kuongeza motisha, ufanisi na kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi na kuifanya sekta ya afya ya Serikali kuwa kimbilio la wataalamu hao badala ya kukimbilia sekta binafsi.

Waziri huyo ametoa maelekezo hayo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk Seif Shekalaghe na Katibu Mkuu wa Tamisemi, Adolf Ndunguru leo Jumatatu, Januari 5, 2025 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa bodi ya wadhamini, uliyofanyika katika Taasisi ya Saratani ya Ocean road (ORCI) jijini Dar es Salaam.

“Haiwezekani na haikubaliki kwa daktari aliyesoma kwa miaka 10 hadi 15 kulipwa sawa na daktari aliye ngazi ya kati kitaaluma hili sio suala la upendeleo….” amesema.

Ameongeza: “Malipo ya madaktari waliopo chini ya Wizara ya Afya na Tamisemi kulipwa viwango tofauti sio jambo la haki akihimiza jambo hilo lazima lirekebishwe.

“Natoa maelekezo katibu mkuu Wizara ya Afya na Tamisemi wafanyie kazi haya mara moja kufanya mapitio ya kina ya malipo ya madaktari kulingana na elimu na ubingwa na ubingwa bobezi,” amesema.

Amesema mapendekezo watakayoandaa viongozi hao kuhusu mapitio ya mishahara yawasilishwe ofisini kwake na watamuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuyafanyia mapitio mapendekezo hayo.

Mchengerwa amesema watumishi wa sekta ya afya ni nguzo muhimu ya mfumo wa huduma za afya nchini, wanapaswa kuthaminiwa kwa kuboreshewa  maslahi yao kulingana na mazingira na mzigo wa kazi wanaoubeba.

Waziri Mchengerwa amesema Serikali inaendelea kusikiliza changamoto za watumishi wa afya  na iko tayari kuchukua hatua stahiki kwa lengo la kuwajengea mazingira bora ya kazi na kuboresha huduma kwa wananchi.

Hatua hiyo amesema ni sehemu ya utekelezaji wa sera na Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) pamoja na dhamira ya Serikali ya Rais Samia kuimarisha huduma za afya kama msingi wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

Awali, akizungumza kabla ya uzinduzi wa bodi hiyo, Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk Omary Ugubuyu amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine, imeongeza  juhudi  kuwafikia wananchi kupitia kampeni za uhamasishaji kwenye jamii ili kujitokeza na kupima kupata matibabu.

“Kama ilivyokuwa kwa Ukimwi, awali watu waliogopa kupima lakini leo hali imebadilika hivyohivyo tunahitaji kuondoa hofu na mitazamo hasi kuhusu saratani ili watu wajitokeze mapema,” amesema.

Dk Ugubuyu amesema kila mwaka hutokea wagonjwa 45,000 na vifo 30,000 kila mwaka.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Profesa Ephata Kaaya amesema katika kuimarisha huduma za uchunguzi wa magonjwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa, taasisi hiyo imenunua mashine za kisasa ambazo zimeanza kutoa huduma.

“Awali taasisi ilikuwa ikihudumia wagonjwa wachache kwa siku, lakini sasa imeongeza uwezo wa kuhudumia wagonjwa kati ya watano hadi sita kwa siku, na matarajio ni kufikia wagonjwa zaidi ya 20 kwa siku ifikapo Juni mwaka huu.

“Kutokana na uwekezaji huo mkubwa, taasisi imeshuhudia ongezeko la wagonjwa kutoka nje ya nchi, ambapo idadi imeongezeka kutoka wagonjwa sita mwaka wa fedha 2021/2022 hadi kufikia wagonjwa 76 kwa sasa, hatua inayotajwa kuwa mafanikio makubwa,” amesema.