Upelelezi wakwamisha kesi ya mauaji ya Mobe

Musoma. Kesi ya mauaji ya Rhoda Mobe (42) aliyekuwa mkazi wa Kijiji cha Burunga Wilaya ya Serengeti mkoani Mara imeahirishwa hadi Januari 19, 2026 kwa kuwa upelelezi haujakamilika.

Kesi hiyo ambayo leo Jumatatu Januari 5, 2026  ni mara ya tatu kusomwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma  inahusisha  washtakiwa wawili, mmoja akiwa ni mwalimu wa shule ya msingi.

Watuhumiwa hao ni Marco Maginga (45) ambaye ni mwalimu na mkazi wa Jiji Mbeya na Mwita Maginga (45) ambaye ni mkulima na mkazi wa Wilaya ya Tarime mkoani Mara.

Akiahirisha kesi hiyo,Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Eugenia Rujwahuka amesema upande wa mashtaka umeeleza kuwa, upelelezi bado haujakamilika hivyo kuomba kupangiwa tarehe nyingine.

“Upande wa mashtaka hawapo mahakamani leo, wametoa taarifa kuomba tarehe nyingine kwa njia ya mfumo na kwa sababu tunaahirisha kwa muda wa siku 14 hivyo tarehe ya kesi hii kutajwa tena itakuwa Januari 19,2026,”amesema Rujwahuka.

Wakili wa utetezi, Mluge  Fabian ameomba kuharakishwa kwa upelelezi ili kuruhusu hatua zingine kuendelea kwa maelezo kuwa wateja wake wamekaa ndani kwa muda mrefu.

“Mtuhumiwa wa kwanza alikamatwa Oktoba 29,2025 na wa pili alikamatwa Novemba 13,2025 na wote walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Desemba 12,2025 huu ni muda mrefu sana naomba upelelezi ukamilike ili tuendelee na hatua zingine,” amesema

Kwa mara ya kwanza watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani Desemba 12,2025 na kufunguliwa shauri lenye namba 23/12/2025.

Ilielezwa kuwa watununiwa hao wanadaiwa kumuua  Mobe kwa kumkatakata  kwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake baada ya kumvamia nyumbani kwake kijijini Burunga.

Tukio hilo lilitokea Oktoba 23,2025 usiku nyumbani kwa Mobe.