Usajili dirisha dogo, Mashujaa yamsikilizia Mayanga

MABOSI wa Mashujaa FC ya Kigoma bado wanakuna vichwa kuhusu usajili wa dirisha dogo, huku wakisisitiza kwamba wanasubiri ripoti ya benchi la ufundi ili kuwa na uhakika wa nini kifanyike wakati huu.

Mashujaa FC imeanza vyema Ligi Kuu Bara msimu huu ikikamata nafasi ya nne ikiwa na alama 13 katika michezo tisa, huku ikiwa imeshinda mitatu, droo nne na kupoteza miwili. Imefunga mabao matano na kuruhusu manne.

Kipa wa timu hiyo, Erick Johora anaongoza kwa kutoruhusu mabao katika michezo mingi akiwa na clean sheets sita katika michezo tisa, huku akiruhusu bao kwenye michezo mitatu pekee.

Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa klabu hiyo, Ofisa Habari wa Mashujaa, Steven Ndorobo amesema mpaka sasa uongozi haujaona sababu ya kufanya usajili dirisha dogo kwani kikosi chao kimekamilika, lakini benchi la ufundi likihitaji nyongeza ya wachezaji watasikilizwa.

MASHU 01

“Bado tunaendelea kufanya tathmini na kutazama kama kuna mapendekezo yoyote kutoka kwenye benchi la ufundi, na kama yatakuwepo basi usajili utakapofanyika tutafahamishana,” amesema Ndorobo na kuongeza:

“Lakini kwa sasa bado tunafikiri kikosi chetu kimekamilika na bado hatujafikiria na hatujaona sababu ya moja kwa moja kufanya usajili kutokana na namna ambavyo  tunakitazama kikosi chetu.”

Ndorobo amesema timu yao imesharejea kambini na inaendelea na maandalizi katika uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma, huku akisisitiza kwamba pengo la beki wao, Abdulmalik Zakaria aliyetimkia Singida Black Stars halitaiathiri klabu yao.

MASHU 02

“Tumeondokewa na beki wetu Abdulmalik Zakaria, lakini kwenye eneo lake bado tuko na mabeki wannne ambao wanaweza wakafanya hiyo kazi vizuri. Tunaye Baraka Mtui, Frank Magingi na Mohamed Mussa, wote wanaweza kusimama kwenye nafasi yake na wakafanya vizuri,” amesema Ndorobo.

“Naweza nikasema kuondoka kwake kama timu hatukuwa na namna kwa sababu yalikuwa ni makubaliano na mchezaji amekwenda kutafuta maisha sehemu nyingine, ni jambo jema, kwetu sisi tunajivunia mafanikio yake.”