VETA YALEMEWA NA WANAFUNZI, 18000 WAJITOKEZA KUOMBA KUJIUNGA NA MAFUNZO

Na Seif Mangwangi, Arusha 

SERIKALI imeuagiza uongozi wa mamlaka ya vyuo vya ufundi stadi nchini( VETA),  kupanua wigo wa uandaaji wa wakufunzi na walimu tarajali wa mafunzo ya Amali kwaajili ya shule za Sekondari pamoja na vyuo vya ufundi na ufundi stadi.

Agizo hilo limetolewa leo 5 Januari 2025 na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir, katika hotuba yake alipokuwa akizungumza na watumishi wa chuo cha ufundi stadi cha hoteli na utalii Njiro pamoja na viongozi wa VETA kutoka makao makuu.

Wanu amesema chuo cha Veta cha hoteli na utali Njiro kina mchango katika kuandaa rasilimali watu ya kutosha inayokidhi nahitaji ya soko la ajira kwenye sekta hiyo nchini.

“Suala hili litafanikiwa zaidi Kwa kuweka utaratibu mzuri Kwa wahitimu wa chuo hiki kupatiwa mafunzo ya mbinu za ufundishaji na ujifunzaji kwa kushirikiana na chuo cha VETA cha Ualimu wa Ufundi stadi Morogoro(MVTTC),” amesema.

Pia Waziri Wanu amewataka vijana nchini kuchangamkia fursa ya kujiunga na vyuo vya ufundi stadi nchini kupata ujuzi utakaowawezesha kupata ajira katika viwanda vya kati na taasisi mbalimbali nchini.

Kwa upande wake DC Joseph Mkude amesema Serikali inaendelea kuhamasisha vijana kujiunga na chuo cha veta Kwa kuwa ni kiunganishi Kikubwa cha utalii katika Kanda ya kaskazini.

Akitoa taarifa ya chuo, Mkuu wa chuo cha Veta cha mafunzo ya hoteli na utalii Njiro, Magubi Mabelele amesema chuo hicho kilianzishwa rasmi 2010 na 2013 kupata ithibati kutoka mamlaka ya usajili ya Nactivet.

Amesema hoteli iliyoko chuoni hapo imekuwa ikiingiza mapato ambayo yamekuwa yakitumika katika uendeshaji wa gharama za chuo pale ambapo makao makuu inapokuwa imezidiwa.

Aidha amesema chuo hicho kimekuwa kikikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mabweni ya kulala wanafunzi jambo ambalo linawafanya kubuni namna ya kuweza kupokea wanafunzi wote kwa pamoja.

“ Chuo kina uwezo wa kudahili wanachuo 1200 kwa mwaka, kupitia fani tano za usafiri wa utalii, mapokezi, uokaji, upishi na usafi, pia tumekuwa tukitoa udahili kwa wanaotaka mafunzo mafupi pamoja na mafunzo maalum, hata hivyo tunachangamoto ya mabweni,” amesema.

Awali mkurugenzi wa Veta Kanda ya kaskazini Monica Mbele alisema ofisi yake inaendelea na ujenzi wa vyuo nane katika maeneo ya Wilaya katika Miko ya Kanda ya kaskazini ambayo hayakuwa na vyuo hivyo.

Amesema baada ya kukamilika kwa ujenzi wa vyuo hivyo, Veta Kanda ya kaskazini itakuwa na jumla ya vyuo 22 na kuongeza idadi kubwa ya wahitimu.

Aidha amesema vyuo hivyo vina changamoto ya walimu kwa fani mbalimbali ikiwemo lugha, vifaa ikiwemo magari kwaajili ya waongoza watalii, kutokuwa na karakana ya fani ya utalii, upungufu wa hosteli na kulazimu vijana wengi kupanga mtaani, 

Mkurugenzi wa VETA CPA Anthony Kasore amesema veta ina vyuo 80 katika Wilaya na Mikoa mbalimbali nchini,  na vingine vimeendelea kujengwa.

Amesema VETA  imeendelea kuongeza wigo wa ushirikiano na wadau wa nje ambao wamekuwa wakileta wanafunzi na kuwalipia Moja Kwa Moja kupitia kampuni zao ambapo Kwa Veta Arusha inapokea wanafunzi 80 wa Moja Kwa Moja kutoka Kwa wadau hao.

Amesema Hadi kufikia 2028 veta inataka kuwa na watumishi 4148 na hivi sasa wako watumishi 2100 na kuishukuru Serikali kuzipatia kibali cha kuajiri watumishi 500 ambapo kati yake wakifunzi ni asilimia70.

“ Mwaka huu tumepokea maombi ya wanafunzi jumla 18,000 na uwezo Wetu ni kuchukua  wanafunzi 14000 lakini tumelazimika kuchukua wanafunzi wote., hata hivyo Vijana 1000 wataanza masomo ya jioni Ili kuwezesha wote wasome,”amesema.

Mkurugenzi Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia anayeshughulikia mafunzo na ubunifu , Prof Fredrick Salukele amesema lengo la chuo hiki cha utalii ni kuongeza mapato na kupunguza utegemezi wa Wizara.