Dar es Salaam. Ili kutekeleza azma ya Serikali inayolenga kuwezesha matumizi ya tehama katika kujifunzia na kufundishia kuanzia ngazi ya shule za sekondari, walimu 606 kutoka mikoa yote ya Tanzania wanatarajiwa kunufaika na mafunzo ya siku tano ili wawe wabobezi katika eneo hilo.
Ndani ya siku hizo, baadhi ya walimu watajifunza namna ya kutumia vishikwambi katika ufundishaji, huku wengine wakijifunza namna ya kufanya marekebisho ya vifaa mbalimbali vya Tehama vilivyopo katika shule zao.
Akizungumza leo Jumatatu, Januari 5, 2026, wakati akifungua mafunzo hayo, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, amesema mafunzo hayo yatakuwa na mchango mkubwa katika kuwajengea uwezo walimu kutumia teknolojia ili waweze kuwapatia wanafunzi maarifa kwa urahisi.
Hiyo ni kwa sababu mafunzo hayo yatafanyika kwa nadharia na vitendo, hali itakayowezesha matumizi yenye tija ya vifaa vya Tehama vilivyopo shule mbalimbali nchini.
Amesema Serikali inatarajia kuona matumizi ya Tehama yanakuwa zana muhimu katika ufundishaji, michoro, picha na vitendanishi mbalimbali katika masomo, na kuongeza mkazo katika masomo ya hisabati, sayansi na Tehama.
“Nitoe wito kwa kila mmoja aliyepata nafasi hii kuweka mkazo katika kile mtakachofundishwa, niwasisitize kuwa wabunifu, kuwajibika na kuhakikisha matumizi ya Tehama yanakuwa chanzo muhimu cha wanafunzi wetu kufanya vizuri, bila kujali umbali walionao au uwepo wa shule, ama ipo mjini au vijijini,” amesema.
Amesema mafunzo hayo ni tafsiri ya sera ya elimu ya mwaka 2014, toleo la mwaka 2023, katika kujengea uwezo walimu wa kutumia Tehama katika ufundishaji na kufanya marekebisho ya vifaa vilivyopo katika shule husika.
Amesema mafunzo hayo yatapunguza gharama za matengenezo madogomadogo ya vifaa vilivyopo katika shule mbalimbali.
“Mafunzo husika pia yamezingatia sera ya elimu ambapo tunaendelea kuweka mkazo katika ujenzi wa maabara za sayansi na teknolojia ya habari na mawasiliano, ili kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji wa masomo ya sayansi, hisabati na teknolojia,” amesema.
Amesema haya yanafanyika wakati wizara inaendelea kuangalia namna ya kuimarisha ufundishaji wa masomo ya hisabati, sayansi na teknolojia kwa ngazi zote za elimu na kuhamasisha matumizi ya teknolojia wakati wa ufundishaji.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu, Fatma Mabrouk Khamis, amesema Tehama si somo la ziada tena, bali ni la msingi katika kuandaa wanafunzi kwa elimu ya juu, ufundi, ajira na ubunifu.
Amesema mafunzo hayo yanatolewa ili kuimarisha ufundishaji wa Tehama kwa msingi wa vitendo na matumizi halisi ya vifaa vinavyohitajika, kutumia Tehama kama nyenzo ya kujifunzia na kuandaa wanafunzi kuwa wabunifu, wabobezi wa teknolojia na watatuzi wa changamoto za kijamii.
“Kama wizara, tutaendelea kutoa msaada unaohitajika ili tuweze kufikia malengo ya kidijitali yaliyoapangwa, na kuandaa rasilimali watu wanaohitajika. Nawasihi walimu mnaoshiriki mafunzo haya kushiriki kikamilifu na maarifa mtakayopewa mkayafanyie kazi,” amesema.
Naye Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano Kwa Wote (UCSAF), Peter Mwasalyanda, amesema katika mwaka huu walimu 606 watapatiwa mafunzo hayo, wakiwa wanatoka mikoa yote Tanzania.
Idadi hiyo ni ongezeko kutoka walimu 300 walionufaika na mradi huo mwaka jana, baada ya Serikali kuongeza bajeti.
“Vituo vinavyotumika kutoa mafunzo haya ni vitatu, kimoja hapa Dar es Salaam kupitia Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), wengine wapo Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), na wengine Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM). Kila kituo kina walimu 202, na kati ya wote, 100 wametoka Zanzibar,” amesema.
Amesema mbali na mafunzo hayo, UCSAF imekuwa ikitekeleza miradi inayohusiana na shughuli hiyo, ikiwemo kuboresha shule kwa kuzipatia vifaa vya Tehama. Hadi mwaka jana, shule 1,210 zilikuwa zimepatiwa vifaa hivyo.
“Pia tunaendelea na zoezi hili, kwa sasa shule 52 zinakidhiwa maabara za kompyuta, na mkandarasi anaendelea na kazi,” amesema.
Mwakilishi wa walimu wanaopewa mafunzo hayo, Fumu Khatibu Fumu kutoka Sekondari ya Mikindani Zanzibar, ameahidi kuwa wataonesha kwa vitendo yale waliyofundishwa katika mafunzo hayo.
“Tunaahidi kuwa tutakwenda kufanyia kazi kile tunachofundishwa, kwani matumizi ya tehama mashuleni yameshika kasi, ikiwemo ya Akili Unde,” amesema.
