Morogoro. Mtawala wa kimila wa Waluguru Manispaa ya Morogoro, Chifu Lukwele wa Nne (Mdimang’mbe), amesema wanajiandaa kufanya tambiko la jadi kwenye makaburi ya waanzilishi wa mji huo, lenye lengo la kuwakumbuka, kuimarisha mshikamano wa kijamii na kuliombea taifa amani.
Tambiko hilo, linalotarajiwa kufanyika Januari 11, 2026, ni sehemu ya juhudi za kulinda historia na kuhuisha thamani ya mila na desturi za asili za kabila la Waluguru, ambazo zimekuwa msingi wa utambulisho wa jamii hiyo kwa vizazi vingi.
Akizungumza na Mwananchi leo, Januari 5, 2026, mjini hapa, amesema tambiko hilo si tukio la kawaida, bali ni ibada ya kimila yenye mizizi ya kihistoria, inayolenga kuomba utulivu katika jamii na kuepusha balaa.
Chifu Lukwele amesema hilo ni tambiko la sita tangu kufufuliwa kwake, likiwa na dhamira ya kuwakumbuka waanzilishi wa Morogoro na kuliombea taifa baraka, amani, mshikamano na mustakabali mwema wa kizazi cha sasa na kijacho, ili kuzuia misukosuko ya kijamii na kisiasa.
Amesema kabila la Waluguru lina zaidi ya koo 50, ambazo zitawakilishwa na viongozi wao katika tambiko hilo, pamoja na viongozi wa Serikali na wadau wa mila na utamaduni kutoka ndani na nje ya Manispaa ya Morogoro.
Mtawala wa kimila wa waluguru Manispaa ya Morogoro, Chifu Lukwele wa Nne (Mdimang’mbe). Picha na Juma Mtanda.
“Tukio hilo litafanyika katika Uwanja wa Gofu, chini ya mti wa Mtamba, uliokuwa ukitumiwa na wazee wa kale kuomba dua za kuilinda jamii dhidi ya mikosi na mabalaa,” amesema Chifu Lukwele.
Mkazi wa Kata ya Kingo, Manispaa ya Morogoro, Sophia Mapunda, amesema matambiko ya kimila yana mchango mkubwa katika kulinda urithi wa kitamaduni na kuimarisha mshikamano wa kijamii.
“Utamaduni ni nguzo ya maadili na umoja. Tambiko hili linatukumbusha kuwa maendeleo ya kweli hayawezi kupatikana bila kuheshimu historia, mila na tamaduni zetu,” amesema Sophia.
Kwa upande wa Mratibu wa tambiko hilo, Thadei Hafigwa, amesema maandalizi yanaendelea vizuri, huku Januari 10 kukitarajiwa kufanyika ziara ya kijamii ya kutembelea na kufanya usafi katika makaburi ya kihistoria ya Kichangani, Msamvu, SUA na Mtawala.
Hafigwa amesema Mkuu wa Wilaya ya Morogoro anatarajiwa kushiriki ziara hiyo kama sehemu ya kujifunza historia ya waanzilishi wa mji huo, huku Mkuu wa Mkoa akitarajiwa kuwa mgeni rasmi.
“Ni tukio lenye umuhimu mkubwa kwa kizazi cha sasa na ni nyenzo muhimu ya kuendeleza utambulisho wa jamii. Vijana wanapaswa kufahamu mizizi yao, kwa sababu jamii isiyotambua historia yake hupoteza mwelekeo na kuiga tamaduni za kigeni zinazovunja maadili,” amesema Hafigwa.
Akielezea historia ya Morogoro, Mwenyekiti wa Shirika la Wazee wa Mila Mkoa wa Morogoro (Shiwamila), Ramadhani Divunyagale, amesema makaburi hayo yanahifadhi kumbukumbu za watawala wa Morogoro kuanzia mwaka 1850 hadi 1942, yakionesha mfululizo wa uongozi wa jadi na nafasi ya wanawake katika utawala, ikiwemo enzi ya Malkia Simbamwene Dangiro Kisabengo (1865–1873).
Divunyagale amesema mwaka 1942 ulihitimisha rasmi utawala wa kifalme Morogoro, lakini makaburi hayo yameendelea kuwa ushahidi hai wa historia inayopaswa kulindwa.
“Tambiko hili litapambwa na burudani za asili, ikiwemo ngoma ya mbeta, vyakula vya asili na dua maalum za kimila kwa ajili ya kuliombea taifa, viongozi wake na wananchi, ili kuiepusha nchi na majanga ya asili,” amesema Divunyagale.