Dar es Salaam. Upelelezi katika kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha kisha kuiba Klabu ya The Voice Tz Limited, inayowakabili Tumaini Moshi (33) na Gasper Mmari (24), haujakamilika.
Wakili wa Serikali, Harrison Lukosi, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Jumatatu Januari 5, 2026 wakati kesi hiyo ilipotajwa.
Tumaini na Mmari ambao wote ni wakazi wa Kinyerezi Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam wanakabiliwa na shtaka moja la unyang’anyi wa kutumia silaha na kujipatia vitu mbalimbali vyenye thamani ya Sh1.5 bilioni mali ya Klabu hiyo.
Lukosi ametoa taarifa hiyo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki.
“Upelelezi wa kesi hii bado unaendelea na ukikamilika tutaitarifu Mahakama, kutokana na hali hii tunaomba Mahakama yako itupangie tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa,” amedai Lukosi.
Hakimu Nyaki baada ya kusikiliza maelezo hayo, aliahirisha hadi Januari 13, 2026 itakapotajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na shtaka la unyang’anyi wa kutumia silaha linalomkabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria.
Washtakiwa kwa pamoja wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 28915 ya mwaka 2025 yenye shtaka moja la unyang’anyi wa kutumia silaha.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, wanadaiwa Oktoba 29, 2025 eneo la Kinyerezi katika Klabu ya The Voice Tz Limited, walifanya unyang’anyi wa kutumia silaha na kisha kuiba vitu vilivyokuwepo katika klabu hiyo.
Siku hiyo ya tukio, Moshi na Mmari wanadaiwa kuiba viti 350 vya mbao na vya plastiki vikiwa na thamani ya Sh150 milioni.
Pia, wanadaiwa kuiba vifaa vya ofisi vikiwa na thamani ya Sh40 milioni.
Iliendelea kudaiwa kuwa washtakiwa hao wanadaiwa kuiba runinga 57, zikiwa na thamani ya Sh480 milioni.
Pia, wanadaiwa kuiba Music System wenye thamani ya Sh250 na POS mashine ikiwa na thamani ya Sh80milioni,” amedai Rimoy.
Washtakiwa hao wanadaiwa kuiba vyombo vya jikoni nyenye thamani ya Sh 25milioni
“Vile vile, washtakiwa hao wanadaiwa kuiba vifaa vya baa yenye thamani ya Sh15milioni,” inaeleza hati ya mashtaka.
Pia, wanadaiwa kuiba vinywaji mbalimbali vyenye thamani ya Sh518milion pamoja.
Mbali na kuiba vitu hivyo, washtakiwa hao wanadaiwa kuiba Sh16.9milioni.
Jamhuri iliieleza Mahakama kuwa jumla ya vitu vilivyoibiwa vina thamani ya Sh1.5bilioni, mali ya Klabu ya The Voice Tz Limited.
Inadaiwa kuwa kabla ya kutekeleza wizi huo, washtakiwa hao waliwatishia kuwapiga kwa kutumia mawe, fimbo na nondo, watu watatu ambao ni Jammy Galus, Masoud Ahmed na Benedict Katarunga ili waweze kupata vitu hivyo bila kikwazo.
Wakati huo huo, mshtakiwa Nasrim Mkangara anayekabiliwa na kesi ya uhaini katika Mahakama hiyo ataendelea kubaki rumande hadi Januari 13, 2026 kutokana na upelelezi wa kesi hiyo kutokukamilika.
Pia, shtaka la uhaini linalomkabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria.
Kesi hiyo iliitwa kwa ajili ya kutajwa na Wakili wa Serikali Harrison Lukosi ameieleza Mahakama hiyo, mbele ya Hakimu Nyaki kuwa upelelezi bado unaendelea na hivyo kuomba ahirisho.
Hakimu Nyaki alikubaliana na ombi la Jamhuri na kuahirisha kesi hiyo hadi Januari 13, 2026 kwa kutajwa.
Mkangara ni miongoni mwa washtakiwa 48 waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya uhaini mahakamani hapo, hata hivyo Novemba 24, 2025 Mkurugenzi wa Mashtaka nchini ( DPP) aliwafutia mashtaka washtakiwa 47 na kuwaachia huru.
Hata hivyo, siku hiyo wakati washtakiwa hao 47 wakiachiwa huru, mshtakiwa mmoja pekee ndio alisalia katika kesi naye ni Nasrim Laurence Mkangara, ambaye DPP anaendele na mashtaka dhidi yake.
Kwa mara ya kwanza, Mkangara na na wenzake walipandishwa kizimbani Novemba 10, 2025 na kusomewa kesi ya uhaini.
Katika kesi hiyo uchunguzi wa awali (PI) namba 26645 ya mwaka 2025, Mkangara anakabiliwa na mashtaka ya kula njama za kutenda uhalifu wa uhaini na shtaka la uhaini.
Anadaiwa kwa nyakati tofauti kati ya Aprili mosi na Oktoba 29, 2025 alikula njama za kutenda kosa la uhaini.
Katika shtaka la pili, washtakiwa wote walidaiwa kuwa Oktoba 29, 2025 katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, wakiwa chini ya utii wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walitengeza nia kuzuia Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.
Anadaiwa kuwa alitengeneza nia hiyo kwa lengo la kuitisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuithibitisha nia hiyo kwa kusababisha hasara kubwa kwa mali za Serikali zilizokusudiwa kutoa huduma muhimu.