Dar es Salaam. Wawekezaji katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) wameongeza utajiri wao kwa Sh6.12 trilioni mwaka 2025, baada ya mtaji kuongezeka kwa asilimia 34, kutoka Sh17.8trilioni Desemba 2024 hadi Sh23 trilioni Desemba 2025.
Takwimu za soko zinaonesha kuwa Benki ya NMB Plc, KCB Group na CRDB Plc zilimaliza mwaka kama kampuni tatu kubwa zaidi zilizoorodheshwa kwa mtaji wa soko, jambo lililoashiria mabadiliko makubwa ukilinganisha na Desemba 2024, wakati kampuni za bia na bidhaa za walaji zilipoongoza.
Mpaka Desemba 31, 2025, NMB iliibuka kuwa kampuni yenye thamani kubwa zaidi sokoni, ikiwa na mtaji wa soko wa Sh4.2 trilioni. Nafasi hiyo ilichangiwa na kupanda kwa bei ya hisa zake, kutoka Sh5,350 hadi Sh8,410 ndani ya mwaka.
Banki ya KCB Group iliyoorodheshwa pia katika masoko mengine, ambapo thamani yake ya soko nayo iliongezeka maradufu hadi Sh4.01 trilioni kutoka Sh2.31 trilioni mwaka mmoja uliopita, baada ya bei ya hisa kupanda kutoka Sh780 hadi Sh1,350.
Kadhalika Benki ya CRDB ilirekodi mojawapo ya ongezeko kubwa zaidi la thamani sokoni. Thamani yake iliruka kutoka Sh1.74 trilioni hadi Sh3.99trilioni na kuiinua kutoka nafasi ya tano hadi ya tatu ndani ya mwaka mmoja.
Katika kipindi hicho, bei ya hisa ya benki hiyo nayo ilipanda kutoka Sh670 hadi Sh1,530.
Kampuni ya bia ya East African Breweries Limited (EABL) iliendelea kubaki miongoni mwa kampuni nne bora, ikihitimisha mwaka ikiwa na thamani ya Sh3.29 trilioni, kutoka Sh2.56 trilioni mwaka 2024. Bei ya hisa zake ilipanda hadi Sh4,160 kutoka Sh3,240.
Ingawa kampuni hiyo ya vinywaji ilishuka kwa nafasi moja, thamani yake ya soko iliendelea kuongezeka, ikisaidiwa na biashara tulivu na matarajio bora ya mapato katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Kukamilisha tano bora, Kampuni ya Twiga (Tanzania Portland Cement Company (TPCC), ambayo mtaji wake wa soko uliongezeka zaidi ya mara mbili hadi Sh1.11 trilioni kutoka Sh647 bilioni mwaka mmoja uliopita.
Bei ya hisa za kampuni hiyo zilipanda hadi Sh6,170 kutoka Sh3,600 mwaka uliotangulia.
Mwathirika mkubwa wa mabadiliko hayo ya soko ilikuwa ni Kampuni ya Bia ya Tanzania (TBL). Awali, ikiwa kinara asiye na mpinzani kwa Sh3.22 trilioni mwaka 2024, lakini mtaji wake sokoni ulipungua hadi Sh2.51 trilioni mwaka 2025 jambo lililoisukuma nje ya tano bora. Bei ya hisa zake ilishuka kutoka Sh10,900 hadi Sh8,510 ndani ya mwaka.
Meneja wa mitaji na ushauri katika kampuni ya udalali wa DSE Vertex International Securities, Ahmed Nganya, amesema utekelezaji wa kanuni mpya za biashara umekuwa kichocheo kikubwa cha mabadiliko katika soko la ndani.
Amesema kanuni hizo mpya zimekuwa daraja muhimu kwa wawekezaji wa ndani, ambao ushiriki wao sokoni umeongezeka kwa kiasi kikubwa mwaka huu.
“Mabadiliko ya kimuundo hayajaongeza tu uwazi, bali pia yameimarisha imani ya wawekezaji wadogo wa ndani, na kuwawezesha kushiriki kikamilifu zaidi katika mchakato wa ugunduzi wa bei,” amesema.
DSE ilianzisha kanuni mpya za biashara zilizoanza kutumika Juni 2025, ambapo mabadiliko makubwa yalikuwa ni kuanza kutumia Bei ya Wastani Uliozingatiwa kwa Kiasi cha Mauzo (VWAP) kama bei rasmi ya kufunga biashara.
Hatua hiyo ilibadilisha mfumo wa awali wa kutumia bei ya mwisho iliyofanyiwa biashara, ambao ulikuwa rahisi kuchezewa kupitia miamala ya kiasi kidogo.
Chini ya mfumo mpya, bei ya kufunga inaakisi VWAP ya miamala iliyotekelezwa katika kikao husika, mradi angalau hisa 100 zimeuzwa.
Kanuni hizo pia zilianzisha mipaka ya mabadiliko ya bei kwa ngazi (tiered price caps) kulingana na mtaji wa soko wa kampuni na idadi ya hisa zilizotolewa, hatua iliyoongeza uthabiti na muundo katika mabadiliko ya bei.
Kwa mujibu wa Kanuni ya 212, kikomo cha bei kinawekwa kama asilimia maalum ya bei ya kufunga ya awali, huku viwango vya mabadiliko vikitegemea mtaji wa soko na kiasi cha hisa.
Dhamana zenye mtaji wa soko chini ya Sh1 trilioni zinaruhusiwa kubadilika kwa asilimia 15. Kwa kampuni zenye thamani ya Sh1 trilioni na zaidi, mabadiliko yanazuiliwa hadi asilimia 5 ikiwa zina zaidi ya hisa Sh2 bilioni zilizotolewa na asilimia 2 ikiwa hisa zilizotolewa ziko chini ya Sh2 bilioni.
Nganya ameongeza kuwa, DSE inaakisi mwenendo wa kimataifa wa uwekezaji na umeanza kupungua katika baadhi ya bidhaa ikiwamo vinywaji vikali na sigara.
Amesema mtazamo huo wa kimataifa umefika pia katika soko la ndani, akieleza kupoa kwa mvuto wa vigogo wa jadi kama TBL na TCC, huku mitaji ikihamishwa kuelekea sekta ya benki.
“Mvuto wa benki mwaka 2025 haukuwa kwa wachache tu bali sekta nzima, ambapo benki kubwa na ndogo ziliona thamani zao zikirekebishwa kwenda juu,” amesema.
Takwimu za soko zinaonesha kuwa, hata benki ndogo za jamii zilipata mafanikio makubwa.
Mathalani Mkombozi Commercial Bank (MKCB) ilirekodi ongezeko kubwa la bei ya hisa kutoka Sh540 hadi Sh2,710, huku za Mwalimu Commercial Bank (MCB) nazo zilipanda kutoka Sh310 hadi Sh460.
Meneja wa ushauri na tafiti katika wa Kampunia ya Zan Securities Limited, Isaac Lubeja amesema utawala wa hisa za benki ni kielelezo cha moja kwa moja cha msukumo mpana wa uchumi wa Tanzania.
“Ukuaji huu endelevu umechangiwa na kuongezeka kwa shughuli za biashara, maendeleo ya miundombinu, uzalishaji viwandani na huduma. Kwa benki, uchumi unaokua humaanisha mahitaji makubwa ya mikopo, ongezeko la miamala na mapato imara,” amesema.
Lubeja amesema ubora wa mali katika sekta hiyo umeendelea kuwa mzuri, huku wastani wa mikopo chechefu (NPLs) ukiwa karibu asilimia 3.5, chini ya kiwango cha kisheria cha asilimia 5.
Amesema NPLs ndogo zimepunguza gharama za akiba (provisioning) na kuimarisha mizania, hatua iliyosaidia hisa za benki kutawala kundi la juu la DSE.
“Kupungua kwa provisioning kumeongeza faida na kuimarisha mizania, mambo yote yaliyofanya hisa za benki kuwa kivutio kikubwa kwa wawekezaji,” amesema.
Pia, amesema ongezeko la mtaji wa soko limechangiwa na kuongezeka kwa idadi ya wawekezaji wanaoshiriki katika soko la hisa.
Amesema uelewa mpana wa masuala ya fedha, upatikanaji bora wa majukwaa ya biashara na mtazamo thabiti wa uchumi mkuu uliwahamasisha wawekezaji wa rejareja na taasisi kuongeza uwekezaji wao katika hisa.
Lubeja amesema mabadiliko ya kanuni za biashara na muundo wa soko yaliyoanzishwa mapema Juni mwaka jana yalicheza nafasi muhimu.
Amesema mageuzi hayo, yaliboresha ufanisi wa soko na ugunduzi wa bei na kuruhusu bei za hisa hasa za benki zinazofanyiwa biashara kwa wingi kuakisi vyema misingi ya msingi ya kampuni.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Exodus Advisory, Ramadhani Kagwandi, amesema utendaji wa mwaka ulisukumwa na “injini pacha” yenye nguvu ya mageuzi ya sera na utendaji wa kifedha.
“Kichocheo cha kwanza kilikuwa mageuzi ya kanuni yaliyotumika kuanzia Juni mwaka jana. Kwa miaka mingi, kampuni zetu nyingi za vigogo zilikuwa imara kimsingi lakini zimekwama kiteknolojia. Kanuni hizi mpya zilifungua fursa kubwa,” amesema.
Injini ya pili, amesema ilikuwa nguvu ya misingi ya kampuni, hususan katika sekta ya benki.
“Sekta ya benki haikufanya vizuri tu; ilitawala. Faida za jumla za sekta zilikuwa zinakaribia Sh trilioni 2 mwaka 2025. Rekodi hii ya faida, pamoja na matarajio wazi ya ukuaji zaidi, iliifanya DSE kuwa kivutio kisichozuilika kwa mitaji ya ndani na ya kigeni,” amesema.
Akiongeza uchambuzi, mshauri wa masuala ya fedha, Abdallah Ndele, amesema ukuaji wa haraka wa benki za Tanzania kwa robo mwaka hadi robo mwaka umefanya ziwe daraja la mali linalovutia zaidi katika soko la ndani.
“Katika Tanzania, tuna kundi linalokua la wawekezaji wenye mtazamo wa muda mfupi. Wanatafuta mapato ya haraka na huangalia fursa za kupata faida kwa muda mfupi. Kwa kuwa benki huripoti ukuaji imara kila baada ya miezi mitatu, hutoa ishara za mara kwa mara za ‘kununua’ ambazo wawekezaji hawa huzitafuta,” amesema.
