WAZIRI BASHIRU AGEUKA MBOGO MACHINJIO B’YOMBO KUGEUKA MAZALIO YA POPO

 ……..

CHATO

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dkt. Bashiru Ally, amegeuka mbogo baada ya kutembelea mnada wa upili wa Buzirayombo na kukuta mazingira yasiyo ridhisha ikiwemo uhaba mkubwa wa maji na uchakavu wa machinjio iliyogeuka mazalia ya popo.

Kutokana na hali hiyo, amelazimika kutoa siku 21 kwa uongozi wa mnada huo kufunga pampu ya kusukuma maji kutoka matenki ya juu na chini kuelekea maeneo mbalimbali ikiwemo vyoo vilivyopo eneo hilo.

Akiwa katika mnada huo ambao umejengwa na serikali kwa gharama ya shilingi bilioni 4.8 tangu mwaka 2020, ameonyesha kutoridhishwa na utendaji kazi wa baadhi ya watumishi wa sekta yake ambao wameshindwa kuukamilisha mradi huo licha ya kutegemewa na wananchi wengi.

Kadhalika ameshangazwa na wafanyabiashara wa mifugo kutotumia mzani uliopo kwenye mnada huo licha ya wao kuuza nyama kupitia mizani yao, jambo analodai huenda likawasababishia hasara wao wenyewe au kuwaibia wauzaji wa ng’ombe na mbuzi.

Hata hivyo, amegomea ombi la kuuzindua rasmi mnada huo licha ya kuruhusu kuendelea kufanya kazi kutokana na mapungufu yaliyopo na kudai kuwa hatua ya pili ya ujenzi wake itakapokamilika, huenda atakuja kiongozi mkubwa wa serikali kuuzindua au kwa yeyote atakaye teuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Awali msimamizi mkuu wa mnada wa Upili Buzirayombo, Fedson Pius, amesema ili kuuchechemua mnada huo kuna haja ya kupiga marufuku minada holela ya ng’ombe na mbuzi wilayani humo ili biashara ya Mifugo ifanyike eneo hilo.

Amesema hatua hiyo itasaidia ukusanyaji mapato ya serikali, uhalali wa mifugo wanayoinunua pamoja na ulinzi wa fedha zao wanapokuwa mnadani hapo.

Kadhalika amesema baadhi ya wafanyabiashara na wanunuzi wa ng’ombe kwenye mnada huo waliugomea utaratibu wa kuuziana mifugo kwa kupima uzito kupitia mzani, badala yake waliamua kuendelea kuuziana kwa makadilio ya mwonekano wa mifugo.

Aidha amesema ukosefu wa maji kwenye mnada huo umetokana na uharibifu wa pampu ya kusukuma maji ambayo imekaa muda mrefu pasipo kufanyiwa matengenezo badala yake akaomba inunuliwe nyingine ili kuondoa changamoto hiyo.

Hata hivyo ameainisha changamoto nyingine za upungufu wa miundo mbinu iliyopo eneo hilo, ikiwemo uhaba wa uzio wa ukuta, thamani za ofisi, ukosefu wa vifaa kwenye kliniki ya mifugo pamoja na ukosefu wa nyumba za watumishi.

Akitoa mchango wake mbele ya Waziri huyo, Mbunge wa Jimbo la Chato kusini, Pascal Lutandula, ametumia fursa hiyo kuiomba serikali kubadili mfumo wa utoaji elimu kwa wataalamu wa mifugo ili muda wao mwingi utumike kwa vitendo zaidi badala ya darasani.

Utaratibu huo utaongeza ufanisi wa watumishi hao kuwa na ujuzi wa kutosha katika kuhudumia mifugo katika magonjwa mbalimbali ukilinganisha na sasa ambapo mifugo inatibiwa kwa kubahatisha, kiasi cha baadhi ya wafugaji kuamua kutumia tiba kwa uzoefu wao wenyewe.

                             Mwisho.