Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, amewataka vijana nchini kuwa wazalendo kwa taifa lao na kuilinda amani kwani itakapotoweka ni vigumu kuirudisha.
Balozi Kombo amesema hayo leo Januari 6, 2026, katika mahafali ya 28 ya wahitimu wa Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dk Salim Ahmed Salim (CFR), yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Diamond Jubilee, akihudhurisha na kutunuku shahada kwa wahitimu hao.
Amewataka vijana kulitendea mema taifa lao, kwani hakuna taifa lingine watakaloishi kwa amani na utulivu zaidi ya Tanzania. Amesisitiza umuhimu wa kuilinda amani ili nao wavirithishe vizazi vyao vijavyo.
“Wanangu, niwaombe na kuwasihi sana, kuweni wazalendo kwa taifa lenu. Mnaporejea mtaani, msijihusishe na makundi yasiyolitakia taifa mema kwa kutojihusisha kwenu na vitendo vya kulitia taifa aibu, kuliaibisha au, kama siyo, kulifedhehesha,” amesema.
Pia, amewataka vijana hao kuwa wabunifu kwa kuwa ulimwengu wa leo ni wa kibunifu zaidi na kujiuza katika soko la ajira, ndani na nje ya nchi, hivyo wanapaswa kuwa wabunifu katika shughuli zao zitakazowapatia ajira huku serikali ikiendelea kuweka mazingira wezeshi.
“Teknolojia inakwenda kasi sana. Itumieni ipasavyo kwa maendeleo yenu na taifa kwa jumla ili kujitengenezea ajira na siyo kuitumia katika mambo yasiyofaa na kupoteza muda. Siku hizi kuna suala la akili mnemba. likitumiwa vizuri litakuza uchumi wa kaya na taifa, hivyo kueni wabunifu na kuvuna matunda ya teknolojia,” amesema Kombo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dk Salim Ahmed Salim, Balozi Ramadhan Mwinyi, amewataka wahitimu hao kutobweteka na kiwango cha elimu walichokipata kwa kuwa elimu haina mwisho, hivyo wawe tayari kujiendeleza kimasomo fursa inapopatikana.
“Msiridhike na kutosheka na kiwango hiki cha elimu mlichokipata. Endeleeni kuongeza ujuzi mkikimbizana na kasi ya teknolojia kwa kuwa dunia inakwenda kasi sana na haiwasubiri. Pia, mkawe raia wema huko muendeko, kwa kufanya hivyo mtatuheshimisha wakufunzi wenu, chuo, Serikali na wazazi,” amesema.
Mmoja wa wahitimu katika kituo hicho, Alexander Mwangoka, amesema anapokea ujumbe wa Balozi Kombo kwa mikono miwili, akitambua kwamba yeye kama Mtanzania ana wajibu wa kulinda amani ya nchi yake.
“Ninatarajia kuanza kazi kwa sababu nimehitimu masomo yangu. Sasa, siwezi kufikia ndoto zangu kama hakutakuwa na amani, kwa hiyo ninajiona nina wajibu wa kuhakikisha amani inadumu kwa mustakabali mwema wa nchi yetu,” amesema Mwangoka.
