SIMBA na Azam zinakwenda kukutana Januari 8, 2026 kwenye nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi zikiwa zimepita takribani siku 32 tangu zikutane mara ya mwisho Ligi Kuu Bara na Azam kushinda 2-0.
Hali hiyo imemfanya Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker kutoa kauli inayoonyesha anataka kulipa kisasi cha timu hiyo kupoteza wakati yeye hayupo.
Nusu fainali hiyo itakayochezwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Unguja kuanzia saa 2:15 usiku, Barker amesema itakuwa nafasi nzuri kwake kuangalia kikosi chake kimefikia kiwango gani cha ushindani, lakini kubwa zaidi anahitaji kushinda na kurudisha furaha Msimbazi.
“Nafahamu tulipoteza mechi msimu huu dhidi ya Azam, kukutana na timu kubwa kama hii kipindi hiki kwangu inanipa motisha katika kujenga timu.
“Mechi hiyo itanipa picha ya kwamba tupo wapi hadi sasa katika maandalizi yetu kukabiliana na timu kubwa kama Azam kwa sababu tunafahamu mbele yetu tuna michezo mikubwa ya mashindano inakuja.
“Hata hivyo, ili tufanye vizuri lazima tucheze mchezo wa haraka, tuwe na mbinu bora zitakazorahisisha hiyo kazi. Nina wachezaji mchanganyiko, wachanga na wazoefu, hii inatokana na wengine kukosekana kwa sababu mbalimbali.
“Mpanzu (Elie) amekuja na mmemuona akicheza, bado naendelea kuwaangalia nyota wengine kupitia mashindano haya ambayo yamekuja wakati mzuri kwetu,” amesema Barker.
Simba ilipofungwa 2-0 na Azam Desemba 7, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, kikosi hicho kiliongozwa na Seleman Matola, ikiwa ni siku chache baada ya klabu hiyo kuachana na Dimitar Pantev, kabla ya Barker kutambulishwa Desemba 19, 2025.
