Biashara chuma chakavu inavyoathiri miundombinu ya umeme

Dar es Salaam. Mtendaji Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Lazaro Twange, amesema licha ya Serikali kufanya uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya umeme, changamoto kubwa inayokwamisha juhudi hizo ni biashara ya chuma chakavu, ambayo imekuwa tatizo katika kulinda miundombinu hiyo.

Kauli hiyo alitoa leo Januari 6, 2026 mbele ya Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, aliyeiagiza Tanesco kuweka ulinzi madhubuti wa miundombinu ya umeme kutokana na uwekezaji mkubwa wa fedha za umma kwenye miradi mbalimbali.

Mbali na maagizo hayo pamoja, waziri huyo amesisitiza usimamizi wa miradi mingine inavyoendelea. Alikuwa anakagua vituo vitatu vya kupoza umeme vya Gongolamboto, Kirenyezi na Mabibo, vinavyotarajiwa kukamilika Agosti mwaka huu.

Twange amesema suala la biashara ya chuma chakavu limekuwa kikwazo kikubwa, kwani wahalifu wanaoingilia miundombinu ya umeme huiba vifaa muhimu, na hivyo kusababisha usumbufu na hasara kubwa kwa wananchi.

 “Tumekuwa tukifanya mikutano na wenyeviti wa mitaa hapa Dar es Salaam na mikoa mingine, tukiwaambia wazi  kama watashindwa kuchukua hatua, giza litakuwa karibu na hiyo itakuwa ni hatari kwa wote. Wakati mwingine ni uelewa na kupitia vikao tunawaelimisha wakishuhudia miundombinu ya umeme inaharibiwa bila kuchukua hatua, wanakaribisha giza,” amesema.

Twange amesema kwa sasa taasisi hiyo inaendelea kusimamia miradi mbalimbali ya umeme, yenye thamani ya Sh15 trilioni inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Miradi hiyo inahusisha maboresho ya miundombinu ili kukidhi mahitaji ya ongezeko la watu na shughuli za kiuchumi.

“Lengo kuu ni kuboresha utoaji wa huduma ya umeme kwani watu wanaongezeka na shughuli za kiuchumi nazo zinaongezeka. Serikali haipitishi miradi ya maendeleo ili kuwa kikwazo, bali ili kuhakikisha huduma bora kwa wananchi,” amesema.

Awali, akizungumzia baadhi ya miradi hiyo Waziri Ndejembi amesema ni ya ufungaji transfoma iliyoanza kutekeleza mwaka 2022 inayolenga kuboresha upatikanaji wa huduma ya umeme katika Jiji la Dar es Salaam ambayo serikali imewekeza zaidi ya Sh280 bilioni.

Katika ziara hiyo, amesema Dar es Salaam ni miongoni mwa mikoa inayotumia umeme mkubwa wa zaidi ya megawati 750 ikilinganishwa na Pwani inmayotumia megawati 100.

Amesema jumla ya matumizi katika maeneo haya mawili yanakaribia megawati 800. Kutokana na mahitaji hayo makubwa, wakati mwingine upatikanaji wa huduma ya umeme huathiriwa na hali ya umeme kuwa mdogo (low voltage) hivyo kusababisha usumbufu kwa watumiaji.

“Kufuatia changamoto hizi, Serikali imeanza utekelezaji wa miradi hii ili kuondoa vikwazo katika upatikanaji wa umeme na kusaidia ukuaji wa viwanda,” amesema.

Waziri Ndejembi amefafanua kitolea mfano mradi wa Gongolamboto ambapo transfoma ndogo ya MV50 imebadilishwa na mpya yenye uwezo mkubwa mara tatu imefungwa ili kuhakikisha wananchi wa Mbagala, Kigamboni, na maeneo jirani wanapata huduma bora.

Kuhusu kituo cha kupooza umeme cha Mabibo, Ndejembi amesema kitasaidia kupunguza mzigo wa umeme kwenye Kituo cha Ubungo na kuboresha upatikanaji wa huduma katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam.