SIMBA ilikuwa katika presha moja kubwa ya kutakiwa kutafuta kipa mpya haraka baada ya makipa wawili wa kikosi hicho kuumia kila mmoja kwa wakati wake na kuelezwa wangekaa nje kwa muda mrefu, lakini ghafla Moussa Camara ‘Spiderman’, amefanya vitu vilivyowashtua mabosi na madaktari wa klabu hiyo.
Alichofanya Camara ambaye naye alifanyiwa upasuaji wa goti kwa njia ya kisasa ya kutobolewa na ilielezwa angekuwa nje kwa muda wa wiki 8-10 tangu Novemba mwaka jana, ni kupiga danadana za kutosha hasa ule mguu wa kushoto ambao alifanyiwa upasuaji nchini Morocco.
Taarifa kutoka ndani ya Simba zinasema kuwa, hatua hiyo imewashtua madaktari wanaomfuatilia maendeleo ya kipa huyo wakiona ni kama jamaa anapona kwa haraka tofauti na walichofikiria hapo awali na kuwapa ahueni.
Taarifa huizo zinasema kuwa, mabosi wa klabu hiyo wamepunguza kasi katika kutafuta kipa mpya hasa wa kigeni kutokana na maendeleo hayo ya Camara.
Camara ameshakaa nje kwa takribani miezi miwili kuuguza goti la kulia ambapo aliiacha Simba ikibaki na makipa wawili Yakoub Suleiman ambaye naye aliumia akiwa Morocco na timu ya taifa, Taifa Stars na kuwafanya wekundu hao kusalia na kipa mmoja pekee Hussein Abel aliyepo na kikosi katika michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026.
“Nadhani mmemuona Camara anachezea mpira, hii ni hatua kubwa na madaktari wametuambia kuna hatua za kushtua anazipiga ambazo hawakuzitarajia hapo kabla,” amesema bosi huyo na kuongeza;
“Tulikuwa tunapambana kupata kipa mpya, lakini kwa sasa tunakwenda taratibu tukiangalia hatua za Camara, unajua kwetu kusaini kipa ni kitu cha wiki moja tu inatosha, tulishapiga hatua kubwa kutafuta makipa kilichosalia ni kuamua tu.
“Tukiona kama tunakaribia dirisha kufungwa na bado Camara hajatupa uhakika basi tutasajili kipa haraka ili tusipate shida muda tunao na huo pia ni ushauri uliopitishwa na makocha.”
Wakati Camara maendeleo yake yakiwa hivyo, mwenzake Yakoub amepewa wiki mbili hadi tatu kuangaliwa kabla ya kufanyiwa uamuzi wa upasuaji.
Kuhusu Yakoub alipelekwa kwa madaktari wakubwa pale Morocco na wakashauri kwamba asifanyiwe haraka uamuzi wa upasuaji, amepewa wiki mbili au tatu ili baada ya muda huo itaamuliwa, tunachoshukuru ni kwamba uvimbe wa lile eneo umepotea sana.”
Simba ilikuwa uwanjani jana kumalizana na Fufuni katika mechi ya mwisho ya Kundi B, huku ikiwa na mechi mbili ngumu za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Esperance ya Tunisia watakayocheza nayo kati ya Januari 23 na 30 zitakazoamua hatma ya kutinga robo fainali kutokea kundi D baada ya kupoteza mbili za awali mbele ya Petro Atletico ya Angola na Stade Malien ya Mali.
Simba iliyofika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita na kupoteza mbele ya RS Berkane ya Morocco ilianza kwa kupoteza nyumbani bao 1-0 kisha kulala 2-1 ugenini mbele ya Stade Malien na kuifanya timu hiyo iburuze mkini kundini nyuma ya Esperance yenye pointi mbili, huku Stade na Petro zikiwa na pointi nne kila moja.
