Dida, Suluhu wavunjiwa mikataba Geita Gold

UONGOZI wa Geita Gold umevunja mkataba na wachezaji wawili kipa Deogratius Munishi ‘Dida’ na beki Fredy Juma Sululu baada ya kucheza mechi ya dhidi ya Ken Gold iliyomalizika kwa sare ya mabao 2-2 uwanjani Nyankumbu, Geita.

Katika mechi 13 Dida staa wa zamani wa Simba, Yanga, Azam na Taifa Stars alidaka 12 na kuikosa waliyocheza dhidi ya Songea United.

Alipotafutwa Dida aliyejiunga na timu hiyo kwa usajili wa dirisha dogo msimu uliopita alikiri kuvunjwa kwa mkataba sababu aliyoambiwa na uongozi ni kuwa wanafanya maboresho mzunguko wa pili kwa kuacha wachezaji na kuleta wapya. “Mkataba uliokuwa umebakia ni wa miezi sita, tumeambiwa tutalipwa mshahara wa mwezi mmoja, barua tumepewa mimi na Suluhu juzi Jumatatu saa 10:00 jioni,” amesema Dida na kuongeza:

“Ni kitu cha kawaida katika mpira wa miguu wachezaji kuachwa na kusajiliwa wapya. Wakati najiunga nao msimu uliopita kwa dirisha dogo wapo walioachwa na wengine tuliingia.”

Mbali na hilo, amesema Ligi ya Championship ni tofauti na Ligi Kuu kwani inatumia nguvu: “Utofauti ni timu zilizoko ligi hiyo zina hamu ya kupanda Ligi Kuu. Timu zinawania ubingwa lazima utofauti utakuwepo.”