Fufuni yahamishia hasira Ligi Kuu Zanzibar

WAHENGA wanasema kuvunjika kwa Koleo si mwisho wa uhunzi. Msemo huo ameondoka nao Kocha Mkuu wa Fufuni, Suleiman Mohamed maarufu Mani Gamera au Govinda, baada ya kushuhudia kikosi chake kikiishia hatua ya makundi Kombe la Mapinduzi 2026.

Fufuni iliyoshiriki mashindano hayo kwa mara ya kwanza, ilikuwa kundi B ikianza na sare ya 1-1 dhidi ya Muembe Makumbi City, kisha ikafungwa 2-1 na Simba, huku ikiwa ndiyo timu pekee kutoka Zanzibar katika mashindano hayo kufunga mabao mengi ambayo ni mawili.

Wakati Fufuni ikiwa na mabao mawili, Mlandege, KVZ na Muembe Makumbi City zote zimeishia makundi kwa kufunga bao moja moja, huku Mlandege ikiwa pekee haijapata pointi kutokana na kupoteza mechi zote wakati zingine zikiambulia pointi moja.

Mani Gamera amesema, kushiriki kwao mara ya kwanza Kombe la Mapinduzi kisha kucheza na Simba na kupoteza kwa tofauti ndogo ya mabao, imemfanya kuamini sasa anaweza kucheza na timu yoyote bila wasiwasi, hivyo wapinzani wake kwenye Ligi Kuu Zanzibar wajiandae.

“Katika ligi sisi tupo nafasi ya pili, lakini kwenye michuano hii ya Mapinduzi tumechukua funzo kubwa sana kwamba tunaweza kucheza na yeyote baada ya kukutana na Simba licha ya kupoteza, kikubwa ni kujiimarisha tufikie malengo kwani tulizidiwa kidogo mbinu kutokana na wenzetu wazoefu.

“Niwatoe hofu mashabiki kwamba kwenye Ligi ya Zanzibar tunakwenda kuonyesha kitu zaidi ya hapa tulivyocheza dhidi ya Simba.

“Tunakwenda kwenye ligi kupambana zaidi kwa ari yetu na nguvu zetu tunaamini zitatufikisha katika sehemu tunayoitaka,” amesema Mani Gamera.

Fufuni ikiwa pia ndio msimu wa kwanza inashiriki Ligi Kuu Zanzibar, inakamata nafasi ya pili kwenye msimamo ikiwa na pointi 30, nyuma ya vinara Zimamoto yenye 31, huku duru la kwanza likikamilika.