Hizi hapa sababu mabasi kuikwepa Stendi ya Magufuli

Dar es Salaam. Suala la baadhi ya mabasi ya mikoani kukwepa kuingia Kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo mikoani na nje ya nchi cha Magufuli limekuwa mfupa mgumu huku wadau wa usafirishaji wakitaja sababu inayochangia.

Wadau hao wametaja umbali wa stendi, mgongano wa kisheria na siasa kuwa ni miongoni mwa sababu za hali hiyo.

Wadau hao wamesema haileti maana kulazimika kuingia stendi hiyo iliyopo Mbezi Luis, Dar es Salaam wakati kila kampuni ina ofisi binafsi zenye miundombinu bora ya abiria kukaa, vyoo safi na hata viburudisho, mambo ambayo usingeyapata kwa ukamilifu ukiingia Stendi ya Magufuli.  

Pia, wamesema stendi imejengwa mbali na maeneo ya makazi ya watu waliko abiria, kiasi kwamba nauli ya kufika kituoni inakuwa sawa au zaidi ya ile anayotoa abiria kwenda mkoani, hivyo wengi wanapandia kwenye vituo binafsi.

Wadau wanakuja na sababu hizo, katikati ya matamko mbalimbali ya Serikali kuyataka mabasi yapite kituoni hapo, ili Manispaa ya Ubungo ikusanye mapato yake, hata hivyo, hayakuwahi kutekelezwa.

Kutokana na hatua ya kugonga mwamba kwa juhudi na matamko mbalimbali, Desemba 27, 2025 ilimlazimu Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Reuben Kwagilwa kuunda kamati ya siku 90 kutathmini uendeshaji wa stendi na kubaini sababu za kwanini mabasi yanakwepa kuingia kituoni hapo.

Ingawa Serikali imekuja na hatua hiyo, baadhi ya wadau wa mabasi hayo, waliozungumza na Mwananchi leo Jumatatu, Januari 5, 2026 wameukosoa uamuzi huo wa Serikali, wakisema ni kupoteza fedha kwa kuwa sababu zinajulikana.

Diwani  mmoja wa halmashauri hiyo aliyeomba hifadhi ya jina lake amesema, sheria ndogo za Halmashauri ya Ubungo zinaelekeza mabasi yote ya mikoani yaingie Stendi ya Magufuli kabla ya kuanza safari.

“Kwa ajili ya ukaguzi wa gari unaofanywa na askari wa usalama barabarani na hatua ya pili, halmashauri watanufaika na ushuru wa getini wa basi kutoka,” amesema.

“Hawaingii ni ujeuri tu, hii biashara kama dawa za kulevya, ukitaka kupamaba nao ni kazi, kwani wana nguvu sana na wanasiasa wazito na hawa kuna wakati huwa wanaondoa mawaziri kwa hiyo si jambo jepesi.”

Akizungumza na Mwananchi, Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Priscus John amesema umbali wa stendi husika, muundo wa ujenzi wake na mazingira yanafanya baadhi ya mabasi yasione umuhimu wa kuingia.

Amesema stendi kama ya Magufuli, imejengwa mbali na kitovu cha mji, ambako ndiko abiria wengi wanapatikana.

Abiria wanalazimika kutumia nauli zaidi ya wanayolipa kwenda mkoani kuifuata stendi hiyo.

“Mtu anatoka Chanika kwenda Stendi ya Magufuli nauli ya bajaji Sh20,000 au zaidi, kiasi ambacho wakati mwingine ni sawa na nauli yake ya kwenda mkoani mfano Dar es Salaam hadi Iringa. Huyu hawezi kwenda Magufuli,” amesema.

Kwa sababu ya umbali huo, amesema mabasi yameona yaanzishe vituo binafsi katika maeneo vinayoona kuna idadi kubwa ya abiria vinawapakia na kuanza safari.

Eneo kilipo kituo binafsi na uelekeo wa safari husika, amesema ndio unaoamua basi likaingia stendi kuu au linyooshe moja kwa moja kwenda katika mkoa linakoelekea.

“Sasa unaenda Arusha na kituo chako kiko katikati ya mji, unalazimishwa uende kwanza Stendi ya Magufuli ambako ni mbali badala ya kwenda moja kwa moja kupitia Mwenge, Tegeta na hatimaye kuendelea na safari ndio maana watu wanakwepa,” amesema.

Sababu nyingine, John amesema namna stendi yenyewe ilivyojengwa imeficha ofisi za mabasi kukatia tiketi, jambo linalotoa nafasi kwa wapigadebe kufanya michezo michafu.

Kwa namna stendi hiyo ilivyo, amesema abiria akifika anaanza kuonana na maduka na baa badala ya ofisi za kukatia tiketi, hapo ndipo wanapokutana na wapiga debe na kuanza kutapeliwa.

“Ilipaswa kuwa abiria akifika tu stendi anakutana na ofisi za mabasi za kukatia tiketi anakwenda kukata tiketi, lakini akikutana na mpigadebe anamtapeli na hatimaye basi linapoteza abiria,” amesema.

Pamoja na ushuru wanaotozwa, amesema stendi hizo ndani yake zina mrundikano wa watu wasio na cha kufanya, uchafu na hata vyoo vichafu kiasi kwamba baadhi ya abiria wanaogopa kuingia.

Hata hivyo, amesema sio kwamba hakuna mapato yanayotolewa, bali Serikali yenyewe haijaweka mifumo imara ya kuyakusanya mengi yanapotea.

Vituo binafsi ndio tatizo

Mwenyekiti wa Umoja wa Madereva wa Mabasi Tanzania (Uwamata), Majura Kafumu ameeleza kampuni nyingi za mabasi zinamiliki vituo binafsi nje ya Kituo Kikuu cha Magufuli.

Vituo hivyo, amesema ndivyo vinavyosababisha mabasi yasiingie Magufuli kwa kuwa yanapakia hukohuko abiria na kuanza safari.

“Ilikuwa vema vituo vya Chanika viruhusiwe kwa sababu ni mbali na Dar es Salaam, lakini sioni sababu za msingi kujenga kituo kidogo Shekilango badala ya gari kukaa kituoni pale Magufuli,” amesema.

Ameeleza kulipaswa kuwepo utaratibu wa usafiri wa kuwakusanya abiria kutoka waliko na kuwapeleka kituo kikuu na sio wakusanywe na mabasi yenyewe.

“Tutaendelea kushuhudia maajabu kuona vituo binafsi vinajengwa hadi Kariakoo ilhali tuliondoa Ubungo kwa kuwa palionekana hapafai tukahamisha ili kupunguza msongamano,” amesema.

Hata hivyo, ameeleza kushangazwa na hatua ya Serikali kuunda kamati, akisema inafanyaje hivyo wakati tayari kuna amri ya mabasi kuingia katika stendi.

Amesema wakati wa ujenzi wa kituo hicho, waliaminishwa kitakuwa cha kimataifa na kujengwa kwake kulionekana kutakuwa na faida, lakini iweje sasa yote hayo yamekuwa kinyume chake.

Amesema wameshasikia matamko lukuki kutoka kwa viongozi mbalimbali akiwamo Mkuu wa Mkoa, Albert Chalamila, lakini yameshindwaje kutekelezwa.

Tatizo ushindani wa kibiashara

Ukiacha sababu nyingine, ushindani wa kibiashara ni jambo lingine lililotajwa kuwa kiini cha mabasi kukwepa kuanzia safari zao au kuingia katika kituo hicho, kama inavyoelezwa na mmoja wa waliowahi kuwa maofisa wa Stendi ya Magufuli.

Amesema baadhi ya kampuni za mabasi zina vituo nje ya Magufuli, huko vinapata abiria wengi, anayesubiri kituo kikuu haambulii chochote, ndio maana wote wanaona wawe na vituo binafsi nje.

“Wasafirishaji wako tayari kuingia Magufuli, lakini kwa sharti kwamba mabasi yote yaanzie Magufuli,” amesema.

Amesema hatua ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) kuruhusu kampuni za mabasi kuwa na vituo binafsi inakinzana na amri ya halmashauri ya mabasi kuingia katika Kituo cha Magufuli.

Kwa sababu ya ruhusa ya Latra, amesema kila kampuni imenunua maeneo yao kwa ajili ya kuanzisha vituo ili vikusanye abiria mijini.

Ameeleza kikubwa ni siasa kwani kuna hofu kwamba, viongozi wa chini wakiwasimamia kwa dhati wamiliki wa mabasi kuhakikisha wanapitisha magari kituoni hapo watagoma na kuleta taharuki.

“Ili isimamiwe litoke agizo kutoka juu hasa kwa Rais na kiongozi wa chini atafanya kwa sababu atakuwa na uhakika kwamba haitamuathiri,” amesema.

Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Habib Suluo simu yake iliita bila majibu. Hata Mkurugenzi wa Latra, Johansen Kahatano simu yake haikupokewa.