Ishu ya straika mpya, Pedro apewa rungu Yanga SC

KIKOSI cha Yanga kinashuka uwanjani usiku wa leo kumaliza na TRA United katika mechi ya michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026, huku kocha mkuu wa timu hiyo, Pedro Goncalves akiachiwa rungu la kuamua straika gani mpya amshushe Jangwani kwa ajili ya kuongeza nguvu kikosini.

Yanga imekuwa ikipiga hesabu za kushusha straika mpya wa kigeni, huku mezani kwa mabosi hao kukiwa na majina mawili wote kutokea Angola na mabosi hao wameamua kumuacha kocha huyo kuamua nani atue katika dirisha dogo la usajili.

Ndio. Pedro alitua nchini wiki iliyopita akitoka Ureno ambako taarifa za uhakika kutoka ndani ya Yanga ni kwamba kocha huyo amewaambia mabosi wake kuwa jina la mshambuliaji anayemtaka analo.

Kama Yanga itasajili mshambuliaji mpya basi atatoka ndani ya majina hayo mawili, Laurindo Dilson Maria Aurelio ‘Depu’ anayeitumikia Radomiak Radom ya Poland kwa mkopo akitokea Vojvodina ya Serbia akipewa nafasi kubwa ya kusajiliwa kwa mabingwa hao wa Tanzania.

PED 04

Mwingine ni Jacinto Muondo ‘Gelson’ Dala anayeitumikia Al-Waktah ya nchini Qatar akitokea Rio Ave ya Ureno ambapo mmoja kati ya hao atavaa jezi za Yanga ndani ya wiki chache zijazo.

Mabosi wa Yanga walipeleka majina mawili kwa Pedro akiwamo mshambuliaji kutoka Guinea, lakini Mwanaspoti linafahamu kwamba, kocha huyo raia wa Ureno amemkataa licha ya kukubali ubora wake, akisema ni sawa na kumsajili Prince Dube mwingine kutokana na ubora wao kuwa wa aina moja.

PED 03

Mbali na mshambuliaji huyo wa Guinea, Yanga pia ilikuwa kwenye mazungumzo na mshambuliaji mmmoja wa DR Congo, lakini uamuzi wa Pedro, umesitisha kwa muda harakati za kumchukua.

“Mshambuliaji mpya ataletwa na kocha, hii safari yake aliyorudi ndio ibebeba hatma ya mshambuliaji huyo, alishaleta jina, itoshe kukwambia kwamba mshambuliaji mpya atatokea taifa la Angola,” amesema bosi huyo na kuongeza;

“Kocha amesema ana imani na mshambuliaji huyo anayemtaka akitaka kumtengeneza acheze kulingana na Dube, kuna jina la mtu tulimpa akamkubali, ni mshambuliaji wa Guinea lakini akasema ni mzuri ila anacheza kama Prince akatushauri tumuache.

PED 02

“Mwingine tulikuwa tunapambana naye kutoka Congo, lakini tumelazimika kupunguza kasi ya mazungumzo ili tufanyie kazi hili jina ambalo amelileta.”

Tayari Yanga imeshachukua viungo wawili, Camara Damaro na Marouf Tchakei kutoka Singida Black Stars wakitanguliwa na mshambuliaji Emmanuel Mwanengo kutoka TRA United.

Wachezaji hao walianza kuitumikia timu hiyo katika mechi ya Mapinduzi 2026 dhidi ya KVZ ambapo Mwanengo alianza kikosi cha kwanza na kusababisha bao la pili, huku Damaro na Tchakei wakiingia kipindi cha pili.

PED 01

Leo nyota hao wanaweza kutumika tena wakati Yanga itakapokabiliana na TRA katika mechi ya mwisho ya Kundi C kusaka timu ya kwenda nusu fainali kila moja ikiwa imeshinda mechi moja dhidi ya KVZ na kutofautiana idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa na mshindi ndiye atakayekata tiketi hiyo.