Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa watatu

JESHI la Polisi Mkoa wa Morogoro limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa watatu wanaodaiwa kuhusika katika matukio tofauti ya mauaji na ukatili wa kijinsia yaliyotokea katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi Mkoa Morogoro imesema kuwa Januari 4, 2026 walimkamata Helakimu Joseph Kacheli (50), mkulima na mkazi wa kijiji cha Sesenga, kwa tuhuma za kumuua mkewe, Sofina Alipisini (27), mkulima na mkazi wa Lumbachini.

Inadaiwa kuwa chanzo cha tukio hilo ni wivu wa kimapenzi baada ya tukio, mtuhumiwa alijaribu kujidhuru lakini aliokolewa na kwa sasa anaendelea na matibabu chini ya ulinzi wa Polisi.

Katika tukio jingine, Januari 5, 2026, jeshi hilo lilimkamata Justine Bernad Thomas (42), mkazi wa kijiji cha Sogeambele, kwa tuhuma za kumuua Machafu Magembe Masanja (42) kufuatia ugomvi uliotokana na mauzo ya mpunga yaliyofanywa bila ridhaa ya marehemu.

Wakati huohuo, wilayani Kilombero, Jeshi la Polisi lilimkamata Andrew Joseph Katanga (33), mkulima na mkazi wa Katindiuka, kwa tuhuma za kufanya ukatili wa kijinsia dhidi ya mwanae wa kumzaa mwenye umri wa miaka 14. Tukio hilo linadaiwa kutokea Desemba 31, 2025, na uchunguzi bado unaendelea.

Kufuatia na matukio hayo Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limetoa wito kwa wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi na badala yake kutoa taarifa mapema kwa vyombo vya usalama ili kusaidia kuzuia matukio ya kihalifu kabla hayajaleta madhara makubwa kwa jamii.