New York. Aliyekuwa kiongozi wa Venezuela, Nicolas Maduro, amefikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza nchini Marekani pamoja na mkewe, Cilia Flores, huku akiendelea kusisitiza yeye bado Rais wa Venezuela.
Maduro na mkewe asubuhi ya jana Jumatatu Januari 5, wamesafirishwa kwa helkopta kutoka eneo walilokuwa kizuizini umbali wa nusu kilomita hadi Manhattan ilipo Mahakama.
Maduro na mkewe wamekana mashtaka yote waliyosomewa na hawakuomba dhamana huku akiendelea kusisitiza yeye bado Rais halali wa Venezuela.
Maduro na mkewe walifikishwa mbele ya Mahakama ya New York baada ya kukamatwa katika operesheni ya kijeshi ya Marekani, hatua ambayo mawakili wake wameitaja kuwa “utekaji nyara wa kijeshi” unaokiuka sheria za kimataifa na misingi ya haki.
Wanakabiliwa na mashtaka mazito yanayohusisha dawa za kulevya na silaha, huku wakichagua kwa sasa kutowasilisha ombi la dhamana.
Akiwa mbele ya Jaji Alvin Hellerstein, Maduro alitamka kwa sauti thabiti:“Mimi sina hatia,” na kuongeza kuwa yeye ni “mtu mwema.”
Alipoulizwa kuthibitisha jina lake, alijitambulisha kama Rais wa Venezuela na kudai alikamatwa nyumbani kwake, tamko lililoibua hali ya tahadhari mahakamani.
Jaji Hellerstein alimkumbusha mshtakiwa huyo kuwa si busara kwa mshtakiwa kuzungumza kwa kina katika hatua za awali za kesi, akisema, “kutakuwa na wakati na mahali pa kueleza yote haya.”
Onyo hilo lilikuja huku tafsiri ya lugha ikiendelea, hali ambayo wachambuzi wanasema huifanya Mahakama kuwa na ugumu zaidi kudhibiti maelezo ya mshtakiwa.
Wataalamu wa sheria wanaona hoja ya Maduro kwamba kukamatwa kwake nje ya mipaka ya Marekani kulikiuka sheria, inafanana na hoja iliyowahi kutolewa na aliyekuwa kiongozi wa Panama, Manuel Noriega, zaidi ya miongo mitatu iliyopita.
Noriega alidai uvamizi wa Marekani na kukamatwa kwake vilikiuka sheria za kimataifa na haki za kimsingi.
Licha ya Noriega kukimbilia ubalozi wa Vatican nchini Panama, majeshi ya Marekani baada ya kushindwa kuingia ubalozini waliamua kufunga maspika makubwa kuzunguka ubalozi huo na kupiga muziki kwa sauti kubwa uliomlazimu Noriega kujisalimisha.
Hata hivyo, jana Mahakama zilipuuza hoja hizo za Maduro na kujikita kwenye mashtaka yaliyokuwa kwenye hati ya mashtaka.
Iwapo Mahakama za Marekani hazitabadilisha msimamo huo wa kihistoria, katika kesi ya Maduro bado ni kitendawili.
Wachambuzi wanasema mwelekeo wa kesi hii unaweza kuweka alama muhimu katika mjadala mpana wa mipaka ya mamlaka ya kisheria, haki za kimataifa, na uhusiano wa kisiasa kati ya mataifa.
Kwa sasa, macho ya dunia yanaelekezwa New York, ambako kesi hii inaendelea kuibua maswali mazito si tu kuhusu hatima ya Maduro, bali pia kuhusu nguvu na mipaka ya sheria katika siasa za kimataifa.
