Mbeya. Zaidi ya kaya 21 katika kata za Ilemi na Isyesye, Jimbo la Uyole, Halmashauri ya Jiji la Mbeya, zilizingirwa na maji ya mafuriko kutokana na mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia Januari 5, 2026.
Mvua hiyo imetajwa kuleta madhara ya uharibifu wa mali, vikiwemo vyakula, huku kaya mbili kati ya 21 zikipata hifadhi chini ya uongozi wa Serikali ya mtaa wa Isyesye.
Kufuatia tukio hilo, mbunge wa Uyole, Dk Tulia Ackson, amefanya ziara ya kukagua maeneo yaliyoathirika na mafuriko hayo leo Januari 6, 2026, na kutoa matumaini ya kusaka mwarobaini sambamba na kuonya wananchi kutupa taka ovyo katika msimu huu wa mvua.
Akizungumza na Mwananchi leo Januari 6, 2026, diwani wa Ilemi, Baraka Zambi, amesema katika eneo lake kaya 15 zilizingirwa na maji yaliyosababishwa na mafuriko, huku chanzo kikitajwa kuwa ni mifereji kuziba na kusababisha kukosa mwelekeo wa maji na kuingia kwenye makazi.
“Kaya 15 zilikumbwa na mafuriko usiku wa kuamkia jana kufuatia mvua kubwa kunyesha, na kusababisha baadhi ya mifereji kufurika, maji kusambaa kwenye makazi ya watu. Pia, kuna maeneo yenye mikondo ambayo hutiririsha maji kwenye mpaka wa Kata ya Ilemi na Isyesye,” amesema.
Kwa upande wake, diwani wa Isyesye, Novatus Agustino, amesema katika eneo hilo kaya sita zilizingirwa na maji ya mafuriko, huku mbili zikihifadhiwa chini ya uongozi wa serikali ya mtaa.
“Hali ilikuwa mbaya, lakini kimsingi tumebaini changamoto ni wananchi kujenga kwenye hifadhi za mifereji, jambo linalosababisha maji kukosa mwelekeo na kuingia kwenye makazi,” amesema.
Amesema ili kudhibiti hali hiyo, wanaomba Serikali kufanya tathmini upya ya maeneo ya hifadhi za barabarani na mifereji ya maji ili kuja na suluhisho la kudumu.
Akizungumza baada ya kukagua maeneo yaliyokumbwa na mafuriko, Dk Tulia amewapa wananchi matumaini na kuelekeza kuwasiliana na mamlaka husika za Serikali ili kuchukua hatua za haraka.
Pia, amewataka wananchi kutokubali kujenga katika maeneo yenye changamoto za kujaa maji na kuonya kuiepuka tabia ya kutupa taka ngumu kwenye mifereji.
“Acheni tabia ya kutupa taka kwenye mifereji, ambayo husababisha kuziba na kupelekea maji kuongezeka na kuleta maafa kwa baadhi ya maeneo,” amesema.
Katika hatua nyingine, amesema atahakikisha anasimamia kuona mamlaka husika zinatekeleza wajibu wa kutatua changamoto hiyo, hususani utatuzi wa mifereji mikubwa inayotiririsha maji katika msimu huu wa mvua nyingi.
Mmoja wa wakazi wa Kata ya Ilemi, Jack Stanley, amesema changamoto kubwa katika kipindi hiki cha msimu wa mvua ni wananchi kukiuka sheria na kutumia maeneo kama sehemu ya kutupa taka ngumu, jambo linalozibua mifumo ya maji taka.
